My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, December 18, 2013

AIR TANZANIA YARUDISHA SAFARI ZA NDEGE ZA KWENDA BURUNDI

 
Meneja Rasilimali watu kutoka Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Eliezer Mwasele, akishuka kutoka ndani ya ndege mara baada ya ndege ya Air Tanzania kutua wakati wa uzinduzi wa safari za kwenda Bujumbura- Burundi. Nyuma yake ni aliekuwa Balozi wa Tanzania Burundi, Francis Mndolwa.
 
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk. James Nzagi (kushoto) akiwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Francis Mndolwa (wa pili kushoto) mara baada ya kupokea ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, Air Tanzania, iliyoanza sarai za kwenda Bujumbura mwishoni mwa wiki. Wengine mbele ni baadhi ya mawaziri wa serikali ya Burundi.
 Baadhi ya abiria wakipanda ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania –Air Tanzania- kabla ya kuanza safari ya kuelekea Bujumbura –Burundi, wakati wa uzinduzi wa safari hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
 Baadhi ya viongozi wakisindikiza abiria walioshuka kwenye ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania –Air Tanzania- mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bujumbura- Burundi kama ishara ya uzinduzi rasmi wa safari hizo. Kutoka kushoto ni Waziri wa Burundi wa Afrika Mashariki, Bi Nziyemana Leontine akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk. James Nzagi na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Francis Mndolwa.
Air Tanzania yarudisha safari za ndege za kwenda Burundi
·       Waanza safari za kwenda Mbeya
·       Warejesha safari za Mwanza

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) limezindua rasmi huduma za usafiri wa anga kutoka Dar es Salaam kuelekea Bujumbura, Burundi kwa kupitia mkoani Kigoma, safari hizo zitafanyika mara tatu kwa wiki yaani Jumatano, Ijumaa na Jumapili.
Hatua hiyo imekuja baada ya hali ya amani kutengamaa katika nchi hiyo ya Burundi ambayo ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuilazimu Tanzania kusitisha huduma hizo kwa muda wa miaka 20.
Wakati huo huo, ATCL pia imeanza safari za Dar es Salaam kwenda Mbeya, safari hizo zitafanyika mara nne kwa wiki yaani Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili. imerejesha safari za Dar es Salaam – Mwanza kila siku, safari  zilizoanza rasmi Jumapili iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Bujumbura Burundi katika uzinduzi wa huduma hizo juzi, Meneja Rasilimali watu wa Shirika hilo la ndege, Ndugu Eliezer Mwasele, alisema uzinduzi wa safari hizo utakuwa ni njia mojawapo ya kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi zote mbili.
Alisema kutokana na hali hiyo Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika nchi hiyo ya Burundi, kwani asilimia kubwa ya wafanyabiashara wa nchi za Kongo na Burundi wanatarajiwa kuanza kutumia usafiri huo kwa wingi.
Akizungumzia hatua hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk. James Nzagi, alisema kuanza kwa safari hizo ilikuwa ni ndoto ya siku nyingi ambayo aliipigania na kutamani kuona wananchi wa pande zote mbili wananufaika kwa pamoja.
“Tumefurahi sana kwa kutimiza ndoto hii leo (juzi), kwa sababu sasa uhusiano kati ya nchi hizi mbili unazidi kuimarika hasa ukizingatia tunategemena kibiashara kulingana na fursa zilizopo.
Kwa upande wake, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Francis Mndolwa, alisema kwa kuwa ATCL imefunga mkanda na kuanzisha tena safari hizo, ni vyema ikazingatia muda na kuhakikisha huduma stahiki zinatolewa ili kukuza shirika hilo.
Naye Waziri wa Burundi katika Bunge la Afrika Mashariki, Nziyemana Leontine alisema, “kuanzishwa kwa Air Tanzania kuja Burundi, kutasaidia wananchi wa Burundi, hususani wafanyabiashara kwani walikuwa wanaunganisha ndege kupitia nchi nyingine, lakini sasa hivi wananchi watakuja moja kwa moja. Tunashukuru sana,” alisema.
Naye mmoja wa abiria kutoka Burundi waliopanda ndege hiyo, Dk. Owera Kodime, alisema, kuanzishwa kwa safari hizo kutawapunguzia sana gharama za usafiri wananchi wa Burundi, kwa sababu Tanzania imepunguza gharama kuliko mashirika mengine.
“Tulikuwa tukitumia muda mrefu sana kuzunguka lakini sasa tutaweza kuja moja kwa moja Dar es Salaam, ni hatua nzuri ambayo imetuletea faraja sana Warundi,” alisema.
Kwa upande wa abiria kutoka Tanzania, Joseph Kisaro, alisema, “ Muda mrefu sana kulikuwa hakuna huduma, tangu mwaka 1993 huduma zilikatatika, lakini uongozi wa Tanzania umefanya juhudi baada ya mapigano kuisha. “Tunashukuru ubalozi ulioteuliwa mwaka 2003 kwani ulianza harakati haraka za kurudisha huduma hizi ambazo sasa tumefanikiwa.
“Tunaomba uongozi wa ATCL uangalie pia kuwa na safari za kuelekea Kongo mashariki kwa sababu kuna abiria wengi sana ambao ni wafanyabiashara wanaokuja Tanzania,” alisema

No comments:

Post a Comment

New