My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, November 12, 2014

Kampuni ya simu yamwaga ajira 2,000......Maombi ya kazi Yanaanza kupokelewa kuanzia LEO



KAMPUNI ya simu ya Viettel ya Vietnam inayokua kwa kasi duniani ambayo sasa inahamishia nguvu zake katika soko la Tanzania, imetangaza ajira kwa wasomi wa Tanzania zaidi ya 2,000.
  
Viettel ambayo uongozi wake wa juu ulikutana na Rais Jakaya Kikwete akiwa ziarani nchini Vietnam hivi karibuni na kuahidi kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano nchini, imetangaza nafasi hizo kupitia gazeti la  Habari Leo na Daily News matoleo ya jana.
  
Kwa mujibu wa tangazo hilo, Viettel inahitaji wataalamu wa karibu fani zote, huku kiwango cha chini kabisa cha elimu kikiwa stashahada, yaani diploma.
  
Wafanyakazi wanaohitajika ni wenye ujuzi katika masuala ya rasilimaliwatu, sheria, fedha, uhasibu, masoko, uchumi, mipango, takwimu, uwekezaji, ugavi, usafirishaji, utunzaji wa vifaa, umeme, simu, teknolojia ya habari na mawasiliano, biashara, utawala na uhusiano wa umma.
  
Tangazo hilo limeendelea kuonesha kuwa, waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kuanzia leo kwa njia ya baruapepe, mwombaji akitakiwa kutuma ujumbe unaoomba fomu kupitia anuani za makao makuu na pia mameneja wa kampuni hiyo walioko katika mikoa yote, Tanzania Bara na Zanzibar.
  
Moja ya anuani ya makao makuu inasomeka; viettelrecruiter@ gmail.com, ambapo mtumaji baada ya kuwasilisha ombi lake, atatumiwa fomu maalumu.
  
Mwenyekiti wa Viettel inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam, Nguyen Manh Hung katika mazungumzo yake na Rais Kikwete, alisema kampuni yake inakusudia kuja na huduma bora zitakazomwezesha kila Mtanzania kumiliki simu ya kisasa (Smart phone), kutokana na punguzo kubwa la bei, licha ya ubora wa huduma zake.
  
Aidha, aliahidi Viettel itafunga huduma ya mawasiliano ya intaneti katika kila kijiji nchini, huku taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo vya Polisi vikinufaika kwa kupatiwa huduma hiyo bila malipo yoyote.
  
Kwa mujibu wa Hung, kampuni yake inapanga kupunguza bei ya simu za kawaida hadi kufikia dola za Marekani 15, sawa na Sh 25,000 na kupunguza bei ya smart phone hadi kufikia dola za Marekani 40, sawa na Sh 65,000.
  
Sasa hivi, bei ya simu hizo ni kubwa zaidi ya kiasi hicho kinachokusudiwa.
  
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, kampuni yake itawekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni moja (Sh trilioni 1.7) katika huduma za simu na huduma nyingine nchini Tanzania, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili nyuma ya Peru kupata mfumo wa simu wa kisasa zaidi miongoni mwa nchi ambako kampuni hiyo ina shughuli zake.
  
Alisema ndani ya miaka mitatu tangu kampuni hiyo kuanza shughuli zake nchini, kiasi cha vijiji 4,000 ambavyo kwa sasa havina mawasiliano, vitapatiwa huduma hiyo katika awamu ya kwanza.

No comments:

Post a Comment

New