My Web

Emmanuel

CONTACT

Saturday, December 31, 2011

Dar LIve

Na Luqman Maloto
Baada ya tafsiri iliyotawala muda mrefu kuwa Wilaya ya Temeke, ipo nyuma katika mambo ya burudani ndani ya Jiji la Dar es Salaam, sasa hivi imekuwa tofauti kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi mkubwa wa kisasa wenye hadhi ya kimataifa unaoitwa Dar Live.
Ukumbi huo ambao ni wa kwanza kuwahi kutokea ndani ya Dar es Salaam na Tanzania kwa jumla, umejengwa eneo la Mbagala, Zakhem, wilayani Temeke.
Dar Live, umejengwa na Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises Ltd ambayo imejipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi katika sekta ya habari na uandaaji wa matamasha makubwa kama vile, Mfalme wa Rhymes, Champions Day na mengineyo, bila kusahau lile la kuhamasisha uzalendo kwa Watanzania lililofanyika hivi karibuni.
Akiutambulisha ukumbi huo kwa waandishi wa habari juzi, Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, alisema kuwa Dar Live ni ukumbi wa aina yake, utakaojishughulisha na utoaji wa huduma za matamasha ya muziki, disko, sherehe za harusi, michezo ya watoto, mikutano na vinywaji.
Alisema, ukumbi huo ni fahari ya Mbagala na Temeke yote, hivyo aliwataka wakazi wa eneo hilo kuanza kujivunia, kwani sasa watakuwa wanapata burudani ya uhakika nyumbani, tofauti na mwanzo walipokuwa wanalazimika kufunga safari hadi Wilaya za Kinondoni na Ilala.
“Pamoja na uwepo wa vifaa vya huduma za michezo ya watoto, kingine ni kwamba Dar Live tumefunga jukwaa kubwa la kisasa la kudumu. Jukwaa ambalo linakidhi mahitaji ya shoo yoyote ya kimataifa.
“Jukwaa limekamilika, lina taa za kutosha, sound (muziki) yenye ujazo mkubwa. Siyo kama kumbi nyingine ambazo hulazimika kukodi majukwaa na muziki. Dar Live imekamilika kila idara. Pamoja na yote hayo, pia kuna bwawa la kuogelea,” alisema Mrisho.

WANAMUZIKI WAKUBWA KUPAMBA UZINDUZI
Mrisho alisema kuwa Dar Live utazinduliwa Januari Mosi, 2012, kuanzia saa 4:00 asubuhi na sherehe za uzinduzi zitakamilika saa 6:00 usiku.
Alisema, kufanikisha uzinduzi huo, wanamuziki wakubwa nchini, watafanya shoo kubwa, itakayoendana na hadhi ya ukumbi wenyewe.
Aliwataja wanamuziki watakaotumbuiza siku hiyo kuwa ni Juma Kassim Kiroboto ‘Sir Nature’ na Kundi lake la Wanaume Halisi, mkongwe Joseph Haule ‘Prof. Jay’, Kundi la Gangwe Mob likiongozwa na Haroun Kahena ‘Inspector’ pamoja na vijana chipukizi wakali wa Kundi la JNY Unit.
Aliongeza, kwa upande wa dansi, Bendi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo’, ikiongozwa na Ali Choki ‘Mzee wa Farasi’ itafanya kazi nzuri ikiwatumia rapa Saulo John ‘Ferguson’, wanenguaji Aisha Mbegu ‘Madinda’, Hassan Musa ‘Nyamwela’ na wengine wengi.
Kwa upande wa burudani ya Taarab, Mrisho alisema kuwa Kundi la Jahazi Modern Taaarab, likiongozwa na Mfalme Mzee Yusuf, litasababisha mirindimo ya Pwani.
Mrisho alitaja viingilio vya siku hiyo kuwa ni shilingi 10,000 kwa VIP, kawaida ni shilingi 5,000 na shilingi 1,000 kwa watoto.
“Watoto wao watafurahia uzinduzi kuanzia asubuhi mpaka saa 12:00 jioni, watu wazima wao kazi kwao kusherehekea matunda ya Dar Live mwanzo mwisho,” alisema Mrisho.
Kuna la ziada? Mbagala wapewe nini wakati wao kesho ndiyo Alfa na Omega?

No comments:

Post a Comment

New