My Web

Emmanuel

CONTACT

Thursday, October 24, 2013

JENGA MSINGI IMARA WA BIASHARA YAKO KWA FAIDA ENDELEVU!

tutazungumzia jinsi ya kuwa na msingi imara kwa biashara yako ili idumu kwa muda mrefu na ikuletee faida kwa sasa na siku zijazo!Jambo la kwanza kabla hujaanza ni kuangalia Uwiano wa Thamani wa Biashara yako (The Value Equation).Watu wengi sana huanzisha biashara kabla ya kufanya uwiano mzuri wa thamani kati ya mtaji utakaotumika na faida wanayotarajia kuipata. Kila mtu huwa analifahamu hili akilini mwake kwa kiwango fulani, lakini ni watu wachache ambao hujitaabisha vya kutosha kuangalia uwiano kati ya hizi pande mbili. Mfano, mama anayetaka kuanza biashara ya maandazi kama kitafunwa cha chai asubuhi, huanza kwanza kwa kukokotoa hesabu ya gharama ya unga wa ngano, amira, sukari, mafuta, umeme au mkaa utakaotumika kuivisha maandazi hayo n.k. Baada ya hapo, mama huyu hukokotoa tena mahesabu ya idadi ya maandazi anayoweza kupika, bei atakayouzia na faida atakayoipata kwa kila andazi. Kisha kutokana na utafiti ambao mama huyu atakuwa ameufanya, maamuzi hufanyika, ama kuanza biashara hii au la. Mara nyingi hivi ndivyo ilivyo hata kwa biashara nyingine nyingi.
Watu huangalia japo juujuu gharama za uendeshaji na hulinganisha na faida inayoweza kupatikana kisha huingia moja kwa moja kwenye biashara.Tatizo kubwa ninaloliona kwa wajasiriamali wengi ni kwamba huwa hawauchukulii uwiano huu kiumakini zaidi. Na hii hufanya wengi kufunga au kushindwa biashara zao baada ya muda mfupi! Kwa kuwa mara nyingi utakuta kuwa mategemeo yao ni tofauti sana na uhalisia wenyewe.
Kwa mfano mtu anayeanzisha shule huwa anakuwa hajaangalia ukweli kwamba kuna miezi ambayo shule zinafungwa lakini waalimu hawaendi likizo, ikiwa ina maana kwamba japo wanafunzi watakuwa majumbani na hawalipi ada, lakini walimu watatakiwa walipwe mishahara kama kawaida. Hii huwasababisha wamiliki wa shule kuhamaki hususan mwaka wa kwanza wa uendeshaji wa shule.Hivyo kuwa na uwiano mzuri wa thamani ni kuyaangalia yote haya. Je, pesa itakuwa inaingia kila siku, kila mwezi au kila baada ya miezi mitatu, sita, tisa au mwaka? Je, kiasi kinachopatikana kitatosha kulipa mishahara na kulipia gharama za uendeshaji?
Baada ya hapo, je, kutakuwa na akiba kwa ajili ya kukuza mtaji na wewe mwenyewe mjasiriamali kulipwa? Mara nyingi ninashangazwa na watu wanaokuja kuniomba ushauri wakiwa tayari na pesa mkononi jinsi ambavyo wanakuwa hawajayaangalia mambo haya kwa kina. Jiulize maswali magumu mengi kadiri uwezavyo kabla hujaamua kuanzisha biashara yako.
1. Je, utanunua bidhaa yako au malighafi kwa kiasi gani? Ni wapi  unaweza kupata kiasi kingi au kikubwa kwa gharama ndogo kadiri uwezavyo?2. Gharama za usafiri ni kiasi gani (kama usafiri unahusika) na utapataje kwa bei ndogo kadiri iwezekanavyo?4. Sehemu yako ya kuendeshea biashara itagharimu kiasi gani? Malipo yatakuwaje? Utakodi? Utapewa bure kwa muda gani (kama inawezekana). Itahitaji matengezo au ukarabati kiasi gani?
5. Utahitaji wafanyakazi wangapi wa kuanza nao? Utawalipa kiasi gani? Au utaanza mwenyewe na mkeo/mumeo/mwanao/nduguyo n.k? Watanufaika vipi na biashara yako? Watafanya kazi kwa muda gani kila siku? Je, watahitaji pesa ya chakula cha mchana au itajumlishwa kwenye mshahara?6. Utahitaji vitendea kazi vipi? Mashine (kama utahitaji)? Kompyuta je? Meza? Viti? Vitagharimu kiasi gani?7. Malipo ya kodi yatakuwa kiasi gani? Utalipa kodi za aina ngapi na kwenye mamlaka aina ngapi?8. Gharama za uendeshaji wa biashara yako kila siku ni kiasi gani? Kama vile umeme, usafiri, maji, usafi, simu n.k?
9. Gharama za uzalishaji/utengezaji au utoaji wa huduma wa siku itakuwa kiasi gani?10. Je, wewe mwenyewe utajilipa kiasi gani kwa wiki, mwezi n.k?

No comments:

Post a Comment

New