My Web

Emmanuel

CONTACT

Thursday, October 24, 2013

JENGA MSINGI IMARA WA BIASHARA YAKO KWA FAIDA ENDELEVU- 3

BAADA ya kuangalia kwa kina kuhusu hatua ya kwanza ya kujenga msingi imara kwa kuangalia uwiano wa thamani ya biashara yako, leo tunaendelea na hatua ya pili na muhimu sana iitwayo kutabirika, kujirudia na uendelevu wa biashara yako  (predictability, repeatability and sustainability).
Ili kuanzisha biashara ambayo itakuja kuwa na mfumo mzuri wenye kuleta faida endelevu, itakupasa kujipanga vizuri kimawazo kabla ya kuanza. Sisemi kwamba bila kufanya hivi huwezi kufanikiwa kwenye biashara au kila aliyefanikiwa leo hii alitumia mfumo ninaoufundisha, hapana!
Baadhi ya wajasiriamali waliofanikiwa walijifunza kutokana na makosa au kwa lugha nyingine, waliiona fursa wakaifanyia kazi na wakajifunza kutokana na makosa. Wengine walipata bahati bwelele. Wengine walitumia njia mbalimbali zisizo sahihi kama wizi, kughushi nyaraka, kukwepa kodi n.k.
Lakini kufanikiwa kibiashara kihalali ni jambo ambalo kwa kizazi tulichonacho, lipo wazi sana kwa mtu yeyote ambaye yupo tayari kujifunza jinsi ya kufanikiwa na yupo tayari kufanya kazi kwa bidii.
Kwa mfano kwa muda huu ninaoandika makala haya, unaweza kwenda kwenye maduka yoyote ya vitabu na ukapata zaidi ya vitabu kumi vya jinsi ya kuanzisha biashara mpya. Unaweza pia kutafuta maarifa kupitia Google kwenye intaneti na ukakutana na tovuti zaidi ya elfu moja zenye ushauri mbalimbali wa jinsi kuanzisha biashara.
Bila shaka baadhi ya hizo tovuti hazitakuwa na ukweli halisi. Pia unaweza kuhudhuria semina nyingi zinazoendeshwa kila mahali siku hizi za jinsi ya kuanza au kuendesha biashara yako. Lakini vilevile kwa kusoma makala haya kila wiki unaweza kujua mambo mengi sana ambayo wasiosoma pengine wanaweza wasifahamu.
Ninachosema hapa ni kwamba, tunaishi katika zama za maarifa na taarifa. Tumezungukwa na maarifa mengi kuliko mahitaji tuliyonayo. Hivyo jipe moyo kwamba chochote unachotaka kukijua leo, inawezekana kabisa ukakijua ili mradi tu ujue wapi kwa kukitafuta. Hakuna siri tena kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo hatukuwa na intaneti, runinga na teknolojia pana kama tuliyonayo sasa hivi. Kwa hiyo uwezekano wa kujua kuhusu ujasiriamali na biashara leo hii ni mkubwa kuliko wakati wowote wa historia ya binadamu. Pia ni rahisi kufanikiwa leo kuliko nyakati zingine zote zilizopita kwa wale ambao siyo wavivu wa kutafuta maarifa na ujuzi wa kila wanachotaka kukifanya!
Sasa tuangalie mambo ambayo yapo kwenye hii hatua ya pili, kutabirika, kujirudia na uendelevu wa mfumo wa biashara yako. Bidhaa unayotaka kuiuza au huduma unayotaka kuitoa ni muhimu ikawa inatabirika, inaweza kujirudia na ni endelevu.
Kwa lugha nyepesi, upatikanaji wa bidhaa au utoaji wa huduma yako unapaswa kuwa wa uhakika, unaoweza kujirudia na utakuwa endelevu kwa muda mrefu.
Kwa mfano, ni vizuri kuwaza kuuza mayai ya kenge au mamba Ulaya kama una uwezo wa kupata wateja kule. Lakini swali la muhimu ni je, unaweza kuwa na hakika wa upatikanaji wa mayai hayo kila wiki au kila yanapohitajiwa na wateja wako? Je, wateja wako wakihitaji makontena kadhaa, utaweza ‘ku-supply?’
I
nawezekana ukawa na uwezo wa kuyapata mayai hayo lakini nadhani utakubaliana na mimi kwamba hiyo haiwezi kuwa kazi rahisi.
Kwa hiyo katika mfano huu, unaona kabisa kwamba bidhaa na biashara hii haiwezi kutabirika, kujirudia au kuwa endelevu kutokana na ugumu wa upatikanaji wake. Biashara inatudai tuwe na uwezo wa kutabiri au tuwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi.
Mfano mwingine ni huu; unaweza kuwa fundi mzuri wa kushona na ukawa na biashara nzuri ya ushonaji nguo na ukapata wateja wanaotaka nguo za harusi ambazo  vitambaa vyake vya kushonea vinapatikana China au nchi za Afrika ya Magharibi.
 Labda kwa sasa huna ‘connection’ na mtu yeyote katika nchi hizo na hata mtaji wa kusafiri na kwenda au kumtuma mtu akuletee kwa sasa huna. Kwa hiyo kama utataka kushona magauni hayo ya harusi kwa sasa utashindwa kutengeneza mfumo ambao ni wa kutabirika, wa kujirudia na endelevu.
Jambo hili halihusu bidhaa peke yake, bali linahusu uuzaji au usambazaji wa bidhaa yako. Kama unataka kufungua mgahawa  kwa mfano, ni muhimu kuhakikisha kuwa wapishi wako watafika kila siku kwa ajili ya kupika. Ikiwa kwa mfano una wapishi wawili lakini kila siku mmoja anatoa kisingizio: “Mara leo naumwa mgongo”, “mtoto anaumwa”, “nimetembelewa na wakwe ghafla” na kadhalika, itakuwa ngumu sana kwa biashara yako ya mgahawa kutabirika, kujirudia na kuwa endelevu”

No comments:

Post a Comment

New