My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, March 26, 2012

KAMA HULI NAFAKA, MBOGA, MATUNDA, UKO HATARINI

ILI mwanadamu awe na afya bora, anapaswa kula kwa wingi vyakula vitokanavyo na nafaka, ale mboga za majani pamoja na matunda, angalau mara kwa mara kama siyo kila siku. Kwa sababu vyakula hivi ndiyo msingi wa afya bora ya kila binadamu.

Kwa mujibu wa wanasayansi wetu, mwili wa binadamu una chembechembe hai (cells) zaidi ya trioni 70. Katika chembechembe hizo ndipo ulipo uhai, zikifa na binadamu naye hufa, zikiwa dhaifu na binadamu naye huwa hivyo hivyo.

Ili chembechembe hizo ziwe hai, zinahitaji kula na chakula chake ni virutubisho tu ambavyo asilimia kubwa na muhimu inapatikana katika vyakula vya nafaka (ambayo haijaondolewa viini lishe). Ndani ya nafaka, kama vile mchele, ngano, mahindi, maharage, n.k., ndiko kunakopatikana virutubisho hivyo.

Madhara ya kuwa na chembechembe dhaifu ni makubwa na unaweza kuyasikia mwenyewe. Kwanza mwili huwa mchovu, usio na nguvu, unapotumia dawa hazifanyi kazi upesi mwilini, kama ni dozi ya malaria, ni lazima utumie zaidi ya moja au dawa kali zaidi! Katika hili baadhi husema fulani ana malaria sugu, lakini ukweli ni kwamba chembechembe zako zimekauka, hazina tena uwezo wa kupenyeza dawa na kutoa sumu mwilini.

MATUNDA NA MBOGAMBOGA
Hili ni kundi la chakula ambalo nalo ni muhimu sana. Baada ya kujenga mwili (chembechembe hai), sasa unahitaji kuulinda ili uwe imara na unaofanya kazi yake sawasawa. Kazi hiyo inafanywa kwa kula matunda na mbogamboga kwa wingi, chakula hiki ndicho kinachojenga mfumo wa kinga ya mwili (Body Immunity System), inayouwezesha mwili wako kujikinga wenyewe dhidi ya maradhi mbalimbali na kukufanya uishi kwa muda mrefu bila kuugua hata malaria.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Dunia (WHO), binadamu anatakiwa kula milo ya matunda na mboga kati ya 5-9 kila siku. Mboga na matunda yana virutubisho muhimu vinavyotoa kinga mwilini (Anti-oxidant) ambayo hupambana na kuondoa viini vya magonjwa (free radicals).

Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya watu hula matunda kwa nadra sana na wengine hawali kabisa! Msimu wa matunda unaingia mpaka unaisha, mtu hajala hata tunda moja au kama kala, basi ya kuhesabu, wengine mpaka waagizwe na daktari, hii ni hatari kwa afya yako na hauutendei haki mwili wako.

Kwa upande wa mboga za majani, hali ni mbaya zaidi, watu hawapendi kula mboga za majani, zinachukuliwa kama chakula cha kimasikini, bila kujua kwamba kwa kuacha kula mboga za majani unayakaribisha maradhi hatari, kama vile saratani, magonjwa ya moyo, n.k.

Ni vizuri ikaeleweka kwamba binadamu hatuwezi kula kama zinavyotaka nafsi zetu, bali tunapaswa kula kama miili yetu inavyotaka. Sisi hatuwezi kuwa muhimu kuliko miili yetu. Kwa mfano, unapopatwa na kiharusi na kupooza mwili, hapo mwili huwa umegoma kufanyakazi na chanzo huwa ni wewe mwenyewe ulishindwa kuupa chakula unachokihitaji ili ujiendeshe wenyewe.

Mwili umeumbwa kama mnyororo, unategemeana sehemu moja na nyingine, sehemu moja inapopatwa na tatizo, mwili mzima unataabika. Maradhi yamekuwa mengi hivi sasa kwa sababu vyakula vinavyouzwa na kuliwa na watu wengi kila siku, hasa mijini, siyo vile vinavyotakiwa na miili yetu. Chukua tahadhari mapema kwa kuzingatia kanuni za ulaji sahihi.

No comments:

Post a Comment

New