My Web

Emmanuel

CONTACT

Saturday, March 10, 2012

Kikwete aingilia kati mgomo wa madaktari


Rais Jakaya Mrisho Kikwete

NI BAADA YA KUAHIRISHA KULIHUTUBIA TAIFA JANA, AFANYA NAO MAZUNGUMZO YA FARAGHA, MBIVU MBICHI LEO
Waandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete jana aliahirisha kulihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na badala yake akaitisha mkutano wa faragha na viongozi wa Chama cha Madaktari (MAT) ambao wanasimamia mgomo wa nchi nzima wakishinikiza kufukuzwa kazi kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.

Rais Kikwete alifanya kikao hicho jana mchana Ikulu, Dar es Salaam huku kukiwa na amri ya Mahakama ya Kazi inayowaamuru madaktari hao kurejea kazini kutokana na maombi yaliyowasilishwa na Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali, juzi.

Hata hivyo, jana madaktari hao waliendelea na mgomo kwa maelezo kuwa hawana taarifa rasmi ya Mahakama hadi walipoitwa Ikulu kuzungumza na Rais Kikwete.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kukutana na madaktari hao ambao wanagoma kwa mara ya pili, ya kwanza ikiwa kuanzia Januari 23, mwaka huu hadi Februari 9 na huu wa pili ulianza rasmi Jumatano iliyopita.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho, hakuna upande wowote uliokuwa tayari kuzungumzia kilichojadiliwa.

Katibu Mkuu wa MAT, Dk Rodrick Kabangila alikataa katakata kuzungumzia kilichojiri kwenye mkutano huo na Rais Kikwete na badala yake akasema leo ataweka kila kitu hadharani.

Usiri huo umeibua mijadala na minong’ono huku baadhi ya wadadisi wa mambo wakisema ama hawakufikia muafaka kwa maana kwamba majadiliano zaidi yanahitajika au hawakukubaliana.

Kulihutubia taifa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema Rais Kikwete alisitisha mpango wake wa kulihutubia taifa jana jioni kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake akasema atafanya hivyo leo asubuhi.

“Ilikuwa alihutubie taifa kupitia kwa wazee wa Dar es Salaam leo (jana) lakini kutokana na Mahakama ya Kazi kuwataka madaktari hao kurejea kazini, analitafakari suala hilo na atazungumza na wazee kesho (leo) saa 5:00 asubuhi,” alisema Sadiki.

Amri ya Mahakama
Akizungumzia amri ya Licha ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuagiza wasitishe mgomo, Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi hawajapelekewa taarifa rasmi... “Hadi sasa unapowasiliana nami sina taarifa. Wewe ndiyo unaniambia.”

Alisema hadi jana mchana Serikali ilikuwa haijawaeleza chochote na kwamba msimamo wao upo palepale.
Jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (NMH), Amana na Temeke hali ilikuwa bado ya kusuasua.
Katika Taasisi ya Mifupa (MOI), baadhi ya ndugu walilazimika kuwahamisha wagonjwa wao na kuwapeleka katika hospitali za binafsi.

Katika baadhi ya ofisi za madaktari katika Hospitali za Temeke na Amana, madaktari wachache walionekana wakihudumia wagonjwa. Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema licha ya mgomo huo, baadhi ya madaktari wanafanya kazi.

Baadhi ya wagonjwa katika hospitali hiyo walisema ni wakati sasa kwa Serikali kuacha malumbano na kutoa tamko linaloeleweka ili kunusuru maisha ya wananchi wake.
“Tunaiomba Serikali ishughulikie suala hili mapema kabla halijaleta maafa kama yaliyotokea awali,” alisema Iddi Moshi aliyelazwa Amana.

Temeke, madaktari walionekana katika maeneo ya hospitali wakipiga soga huku wengine wakiwa katika vyumba vyao vya kutolea huduma wakiwa wamekaa huku wakijisomea vitabu na magazeti.

Maeneo katika hospitali hiyo yaliendelea kuwa wazi huku wahudumu katika mapokezi wakiwashauri wagonjwa kwenda katika hospitali nyingine.

“Nimefika hapa mwanangu anaumwa mwili mzima lakini nilichoambiwa ni kuwa kuna mgomo wa madaktari hivyo wamenitaka nimpeleke hospitali nyingine,” alisema Mkazi wa Kongowe, Zabibu Omary.

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Mtoni Mbuyuni, Asha Abdallah aliyefika hospitalini hapo kwa matibabu ya moyo alisema kwamba ameambiwa hakuna huduma mpaka pale atakaposikia matangazo kuwa huduma zimeanza kutolewa.

Hospitali ya Mwananyamala kulikuwa na mgomo baridi huku uongozi ukisema huduma zote zinatolewa kama kawaida.

Mgogoro
Mgogoro baina ya Serikali na madaktari uliibuka Januari 23 mwaka huu, baada ya kufukuzwa kwa madaktari waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo katika Muhimbili ambao waligoma Januari 4 na 5 wakishinikiza Serikali iwalipe posho zao zilizocheleweshwa kwa kipindi cha miezi miwili.

Januari 12,
MAT kiliitisha mkutano wa dharura wa Baraza Kuu na kujadili hoja kadhaa na kuipa Serikali saa 72 kuwarejesha madaktari hao katika mafunzo Muhimbili kikisema Serikali ndiyo iliyoshindwa kuwalipa fedha zao kwa wakati.

Januari 17
Wizara kupitia kwa Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya ilitoa tamko akipuuza madai ya madaktari hao huku akieleza sababu za kuwatimua Muhimbili kuwa ni kutokana na kuvunja mkataba na mwaajiri wao.

Pia alikionya na kukikumbusha chama hicho kutekeleza majukumu yake kwa mjibu wa katiba yao kwa kushirikiana na Serikali kuimarisha sekta ya afya na wataalamu walio kwenye sekta hiyo kwa manufaa ya nchi badala ya kujihusisha na harakati.

Januari 18
Madaktari walikuja juu wakisema kauli hiyo imedhalilisha taaluma yao na walituma ujumbe wa watu watatu ulioongozwa na Makamu wa Rais wa MAT, Dk Primus Saidia kwenda wizarani kumuita Dk Nkya kwenye mkutano wao na kuwataka wakutane kesho yake.

Januari 19
Madaktari zaidi ya 300 walikusanyika ukumbi wa mikutano wa Don Bosco wakimsubiri, Naibu waziri huyo ambaye nusu saa kabla ya muda uliopangwa kuanza mkutano, alibadili eneo akiwataka wakutane Ukumbi wa Arnautoglu na madaktari hao waligtoma.

Baadaye Dk Nkya alikaririwa na vyombo vya habari akiwataka wawasilishe madai yao kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe).

Januari 20
Ujumbe wa watu watatu ukiongozwa na Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi uliwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu pendekezo la madaktari kutaka naye bila mafanikio.

Januari 23
Walitangaza mgomo na kusema hawako tayari tena kuzungumza na wizara.

Januari 27
Walitangaza kuwakataa viongozi wote wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanzia Waziri, Dk Mponda, Dk Nkya, Katibu Mkuu Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa. Pia Walisoma madai yao kadhaa likiwamo la kumtaka Waziri Mkuukumshauri Rais kuwaondoa Waziri na Naibu wake katika Wizara hiyo kutokana na kushindwa kuwajibika.

Januari 29
Pinda alitoa wito kwa madaktari wote kurejea kazini Januari 30 mwaka huu na ambaye angekaidi angekuwa amejifuta kazi lakini hali ikawa mbaya zaidi.

Februari 9
Pinda alikutana na madaktari Muhimbili na kutangaza kuwasimamisha kazi Nyoni na Dk Mtasiwa akisema suala la Dk Mponda na Dk Nkya lipo nje ya uwezo wake na kwamba amemuachia Rais Kikwete ang'amue.

Februari 29
Rais Kiwete alihutubia Taifa na kueleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa madaktari kusitisha mgomo na kuwataka wawe na subira wakati Serikali inashughulikia madai yao.

Machi Mosi
Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema madaktari hao walikataa kuendelea na kikao cha kamati iliyoundwa na Pinda wakikataa madai yao kujadili kwa kuchangamana na wafanya kazi wengine wa sekta ya Afya.

Machi 3
Madaktari walikutana katika mkutano wao wakufanya tathmini na kisha kutoa siku tatu kwa Waziri Mponda na Naibu wake wawe wamewajibika au kuwajibishwa la sivyo wangeingia kwenye mgomo.

Machi 6
Waziri Mkuu alikutana na waandishi wa habari na kupinga madai ya madaktari hao kutaka Waziri na Naibu wake wawajibike au kuwajibishwa.

Machi 7
Madaktari wakaanza kugoma rasmi ikiwa ni awamu ya pili.

No comments:

Post a Comment

New