My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, March 20, 2012

WAJUA KAMA VYAKULA HATARI NDIYO VINAVYOLIWA KWA WINGI?

WENGI wetu tunafanya kosa kubwa kila siku kwa kula kwa wingi vyakula ambavyo tulipaswa kuvila kwa kiasi kidogo, hii ni kutokana na kutopata elimu ya kutosha kuhusu jambo hili au kwa wengine kupuuzia licha ya kuujua ukweli.
Aina hizo ni zile za Protini (Proteins), mafuta na wanga (Fats & Carbohydrates). Hili ni kundi la vyakula HATARI sana lakini ndilo linalopendwa na watu wengi, unapotumia vyakula vyake unapaswa kuvitumia kwa uchache na uangalifu mkubwa. Kundi hili ndilo linalowaletea matatizo ya kiafya watu wengi.
Vyakula vilivyo katika kundi la protien ni kama vile nyama, mayai, maziwa, n.k na vyakula vilivyo katika kundi la Fats ni vile vyenye mafuta na vinavyopikwa kwa mafuta mengi, kama vile chips, n. k. Vyakula vilivyo katika kundi la wanga (Carbohydrate) ni pamoja na sukari na vyakula vingine vitamu vitamu.

SUALA LA KUZINGATIA
Katika aina za vyakula zilizotajwa hapo juu, tahadhari kubwa inatakiwa ichukuliwe kwa sababu hutakiwi kuacha kabisa kuvila na pia hutakiwi kuvila sana. Binadamu anahitaji Protini mwilini ili kuuwezesha mwili kupata virutubisho muhimu vya kuuendesha mwili wake, halikadhalika mafuta na wanga.
Lakini ni vizuri ukaelewa kwamba kila aina ya chakula iliyotajwa katika kundi hilo la hatari, unaweza pia kuipata kutoka katika kundi lingine la vyakula salama na ukapata virutubisho vyote muhimu.
Katika kundi la nyama, pendelea kula samaki au kuku badala ya nyama ya ng’ombe au nyama yoyote nyekundu (red meat) na usipende kula ngozi, iwe ya samaki au ya kuku, kwani huwa zina mafuta mengi ambayo siyo mazuri kiafya.
Badala ya kula sukari, pendelea kula mboga na matunda ambayo yana sukari ya asili na isiyo na madhara. Au pendelea kutumia asali pahali panapohitaji sukari na ukilazimika kutumia sukari, pendelea sukari nyeusi (brown sugar) kuliko nyeupe na kwa kiasi kidogo sana.
Kundi la chakula cha mafuta, wanga na protini, hutakiwa kuliwa kwa uchache sana na kwa tahadhari kubwa, lakini kwa bahati mbaya sana kundi hili ndilo ambalo linaliwa sana kuliko makundi yenyewe (nafaka, matunda na mboga) na matokeo yake watu wengi wamepatwa na matatizo ya kiafya kama vile kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na matatizo ya unene wa kupindukia.
Baada ya kupatwa na matatizo hayo ya kiafya, wengi wao hivi sasa wameshakatazwa na daktari kuendelea kuvitumia vyakula hivyo na wanapokaidi maagizo wanayopewa, matatizo yao ya kiafya huwa mabaya zaidi na hatimaye kifo. Hivyo wewe kama hujafika huko, badili mfumo wako wa kula kuanzia sasa.
Katika hali halisi na kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), tunapaswa kula zaidi vyakula vitokanavyo na nafaka, matunda na mboga, kisha kula kiwango kidogo sana cha vyakula vitokanavyo na nyama, mafuta na sukari. Kama mgawanyo huo ukiwekwa katika asilimia 100, basi unaweza kuugawa kama ifuatavyo:
Nafaka: 40%
Matunda, Mboga: 35%
Nyama, mayai, maziwa: 15%
Mafuta, Sukari,n.k: 10%
Lakini hali halisi haiko hivyo, maisha wanayoishi watu wengi yamegeuzwa, wanakula sana vyakula vya mafuta, sukari, nyama, mayai. Matokeo yake hivi sasa wanakabiliwa na magonjwa yasiyotibika na kama hawajapatwa, wanajiweka katika hatari ya kupatwa wakati wowote.
Kama ulikuwa hulijui hilo, basi ni vyema ukaanza kubadilika na kuviangalia vyakula katika mtizamo tofauti, achana na vyakula vilivyo katika kundi la hatari na badala yake pendelea kula vyakula vya asili na vilivyosalama, kama kweli unajali afya yako.
Daima kumbukeni, jinsi ulivyo leo, kunatokana na ulivyokula jana na utakavyokuwa kesho, kutatokana na unavyokula leo!

No comments:

Post a Comment

New