My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, March 26, 2012

Nyanya: Dawa kiboko ya minyoo

Minyoo ni wadudu hatari ambao huingia tumboni mwa binadamu na kusababisha matatizo kadhaa ya kiafya. Ukubwa wa minyoo tumboni hutofautiana, kuna minyoo yenye urefu wa kuanzia inchi sita hadi inchi 26, ikitegemea imekaa kwa muda gani tumboni.

Kwa kawaida minyoo huingia tumboni kwa njia kuu mbili, ingawa zipo njia nyingine. Minyoo huingia tumboni kwa kula chakula kisicho salama au kwa njia ya ngozi, hasa kwa watu wanaopenda kutembea na kucheza bila viatu miguuni.

Watoto ndiyo wanao ambukizwa zaidi minyoo kwa njia ya ngozi kutokana na tabia yao ya kupenda kucheza bila viatu, tena wakiwa sehemu zisizo safi. Vile vile mtu anaweza kupata minyoo kwa kunywa maji yasiyo salama au kwa kuumwa na mbu, inzi na hata kwa njia ya kujamiana bila kinga.

Dalili za mtu mwenye minyoo ni pamoja na mtu kuwa na utapiamlo, kuonekana dhaifu na ngozi kupauka, kusumbuliwa na tumbo, kula sana na kusikia njaa muda mfupi baada ya kumaliza kula. Pia mtu mwenye minyoo huwa mwenye hasira kila mara.

TIBA YA NYANYA
Pamoja na tiba mbadala nyingine unazoweza kuzijua, nyanya imepewa nafasi ya kwanza katika kutibu tatizo hili kwa mafanikio makubwa na bila kuleta madhara kwa mtumiaji baada ya kumaliza tiba.

JINSI YA KUTUMIA NYANYA KAMA TIBA
Tayarisha nyanya mbili za ukubwa wa kawaida kwa kuziosha vizuri (inashauriwa uzioshe kwa maji ya moto ili kuua vijidudu, ikiwemo minyoo), zikatekate
Kisha changanya na chumvi pamoja na unga kiasi wa pilipili manga.

Kula mchanganyiko huo wa nyanya, chumvi kidogo na pilipili manga asubuhi kabla ya kunywa chai au kitu chochote. Fanya zoezi hilo mara moja kwa siku, kwa muda wa siku 15 au wiki mbili. Kwa kula nyanya hizo, minyoo wote waliyomo mwilini mwako wataondoka na kuacha tumbo lako safi.

Tiba hii inaweza pia kutumiwa na watoto, lakini kwa watoto wenye umri wa KUANZIA MIAKA MITATU TU na kuendelea, haishauriwi kutumiwa na watoto wadogo chini ya umri huo.

FAIDA NYINGINE ZA NYANYA
Wakati ukitumia nyanya hiyo kama tiba ya minyoo, utakuwa pia unanufaika na faida zingine za kiafya zitokanazo na nyanya, ambazo ni kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya saratani.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizokwisha fanyika, pamoja na virutubisho vingine ilivyonavyo, nyanya ina kirutubisho muhimu na cha kipekee kinachojulikana kwa jina la Lycopene. Kirutubisho hiki kina uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya saratani.

Aina mbalimbali za saratani zinazoweza kuzuilika kwa kula nyanya zimeorodheshwa kuwa ni saratani ya kibofu, saratani ya kizazi, saratani ya njia ya haja kubwa, saratani zote za tumbo, mdomo na saratani ya koo. Nyanya mbichi ndiyo yenye sifa ya kutoa matokeo mazuri.

Ili kujiepusha na kupatwa na minyoo, zingatia usafi, epuka ulaji wa vyakula vya kwenye makopo (refined food), kupenda kunywa juisi zilizowekewa rangi za ladha ya matunda, biskuti, pipi na vyakula vibichi, zikiwemo nyama zisizoiva vizuri.

Ili kujitengenezea kinga dhidi ya minyoo, pendelea kula vitunguu saumu na karoti mara kwa mara, kwani vyakula hivi vina virutubisho ambavyo ni adui mkubwa wa minyoo tumboni. Pia pendelea kunywa maji mengi sana kila siku, maji husaidia kusafisha tumbo, ikiwemo kuondoa minyoo.

No comments:

Post a Comment

New