My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, March 26, 2012

Kitu usichokijua kuhusu ‘juisi ya boksi’- 2

WIKI iliyopita tulianza makala haya kwa kueleza ukweli kuhusu juisi ya boksi ambayo huandikwa asilimia 100 ‘pure fruit juice’ na kusema kwamba haya ni maneno ya kibiashara ambayo hayana ukweli wowote. Sasa endelea...

Aidha, Hamilton anaendelea kueleza mchezo mchafu unaochezwa na watengeneza juisi viwandani kwamba ladha ya juisi hiyo ya machungwa hutofautiana pia kati ya nchi na nchi, kwani viwanda huweka aina ya ladha kwenye chungwa kulingana na vile ambavyo wanapenda watu wa eneo inakokwenda.

Juisi inayotengenezwa kwa ajili ya nchi za Amerika Kaskazini huwa na kiwango kikibuwa cha kirutubisho aina ya ‘ethyl butyrate’, ambacho ni moja ya kemikali inayotumika sana kwenye utengenezaji wa manukato na ladha. Mbali ya kirutubisho hicho kuwa na uwezo wa kutengeneza aina mbalimbali za ladha za matunda, lakini pia hakina gharama (cheap).

HATUA GANI ZA KUCHUKUA SASA?
Kama makala haya yatakuwa yamekushitua na kukushangaza, jua hauko peke yako. Hata hivyo, lengo kubwa la makala haya ni kukufumbua macho ujue juisi unayokunywa siyo salama kiasi gani na uwe na uamuzi wa kuicha au kuendelea kuitumia kwa hiyari yako mwenyewe, lakini siyo kwa kudanganywa na maelezo ya uongo ya kibiashara yanayowekwa juu yake.

Kama ambavyo mwandishi wa kitabu hicho Bi. Hamilton anavyosema: “Lengo la kitabu changu siyo kukataza watu kunywa juisi, isipokuwa kuwafanya wakijue vizuri wanachokinywa. Watu wana haki ya kujua ni kwa kiasi gani utengenezaji wa juisi hivi sasa umekuwa wa kibiashara zaidi, hii itawafanya wawe na maamuzi sahihi kuhusu afya zao.”

Ingawa ni vigumu sana kuepuka ‘kuingizwa mkenge’, lakini unaweza kujiepusha na madhara ya kiafya yatokanayo na unywaji wa juisi hizi ‘feki’ kwa kupendelea kunywa juisi uliyoitayarisha mwenywe nyumbani na kuacha kununua vyakula au vinywaji ‘ready made’, hasa kwa vile ambavyo vinapatikana kwa wingi sokoni.

TAHADHARI
Kwa ujumla matunda na juisi zake zina virutubisho vingi muhimu kwa ustawi wa afya ya binadamu, lakini tahadhari inatolewa kwa wanaopenda kunywa kiasi kingi cha juisi za matunda, hasa juisi ya machungwa ambayo inaelezwa kuwa na sukari nyingi.

Kiasi cha glasi moja ya juisi ya machungwa ina wastani wa gramu 25 za ‘fructose’, (sukari), kiwango ambacho ni cha mwisho kabisa anachotakiwa mtu kutumia kwa siku moja. Hii ina maana kama utakunywa zaidi ya glasi moja pamoja na vinywaji vingine vinavyotumia sukari, kama vile chai, tayari utakuwa umezidisha kiwango kinachopendekezwa kwa siku.

Iwapo utakuwa na tatizo la unene na unahitaji kupunguza uzito, ni vyema ukapunguza sana au ukajiepusha kabisa na uywaji wa juisi za matunda, kwa sababu kiwango cha sukari kilichomo ni zaidi ya wastani unaotakiwa.

Ili upate faida za virutubisho vinavyopatikana kwenye matunda, yakiwemo machungwa, unashauriwa kula matunda hayo kama yalivyo kuliko kukamua juisi na kutupa makapi yake. Inaelezwa kwamba sukari iliyomo kwenye chungwa inapoliwa pamoja na nyama zake (fibre), sukari hiyo huwa haina madhara kwani huweza kujichanganya kwenye mfumo wa damu bila kuleta athari zozote kwa mlaji.

Hivyo ushauri wa ujumla unatolewa kwamba pendelea zaidi kula matunda na mboga za majani kama zilivyo kuliko kunywa juisi zake. Kwa kufanya hivyo utajiepusha na uwezekano wa kusumbuliwa na ugonjwa wa kisukari. Iwapo utakunywa, basi kunywa nusu glasi au isizidi glasi moja kwa siku. Asanteni.

No comments:

Post a Comment

New