My Web

Emmanuel

CONTACT

Friday, August 24, 2012

BBC yaanzishaDira ya Dunia kwenyeTV

IDHAA ya Kiswahili ya BBC imezindua kipindi cha habari cha Dira ya Dunia hapa nchini ambacho kitarushwa moja kwa moja kutoka Londonkupitia Kituo cha Televisheni cha Star(Star TV)
Kipindi hicho cha nusu saa kitakuwa cha kwanza duniani kutangazwa kwa Kiswahili kupitia televisheni ya Star Tv hapa nchini.

Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili, Ali Saleh alisema kipindi hicho cha nusu saa kitaanza kurushwa rasmi Agosti 27,mwaka huu kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa saa 3 usiku kupitia  Star Tv.

Saleh alisema kipindi hicho kitatoa chachu katika matangazo ya Star TV kwa kuwaletea watazamaji wa habari za kiwango cha juu kutoka katika kitovu cha habari za dunia cha BBC-Global News.
“Uzinduzi wa Dira ya Dunia kupitia TV, ni kwenda na mabadiliko tunayoyashuhudia ya jinsi watu wanavyofuatilia habari barani Afrika, na pia mahitaji ya mashabiki wa BBC Idhaa ya Kiswahili,”alisema Saleh na kuongeza.

“Dira ya Dunia itawaletea watazamaji taswira na uchambuzi yakinifu kutoka kwa waandishi wa habari waliotapakaa katika nchi 48 barani Afrika, na hivyo kuleta picha halisi ya bara zima kwa watazamaji wanaozungumza Kiswahili”.

Alisema Dira ya Dunia itatoa taswira halisi ya Afrika, tofauti na jinsi ambavyo bara hili limekuwa likiripotiwa kwa miaka mingi. Kipindi chetu kitakuwa kinashirikisha watazamaji, na pia kuzigatia misingi ya BBC ya muda mrefu ya uhuru, uhakika na bila upendeleo.

Awali Meneja mipango na utafiti wa kampuni ya Sahara Media Group, Nathan Lwehabura, alisema ni heshima kubwa kwa Star TV kujumuisha Dira ya Dunia katika vipindi vyake vya kila siku.
“Ni matumaini yetu kuwa ushirika kati ya BBC na Sahara Media Group utaimarisha matangazo yetu ya TV hasa tunavyoelekea katika matangazo ya kisasa ya mfumo wa dijitali.”alisema Lwehabura.

Lwehabura alisema uanzishaji wa Dira ya Dunia katika TV ni sehemu ya mabadiliko makubwa ya matangazo yaliyofanyika ndani ya BBC mwaka huu barani Afrika, katika TV na redio
Meneja huyo alisema BBC ilirusha matangazo yake ya kwanza barani Afrika zaidi ya miaka 80 iliyopita. Idadi kubwa ya wasikilizaji kwa ujumla kupitia redio na TV inaifanya BBC kuwa shirika kubwa zaidi la kimataifa la utangazaji barani Afrika.

Naye Mhariri wa BBC eneo la Afrika, Solomon Mugera alisema kwa miongo mingi ya utangazaji katika lugha mbalimbali barani Afrika, BBC imejenga uhusiano wa kipekee na wasikilizaji wetu wa redio, kwa kueleza ya Afrika duniani, na kuipeleka dunia barani Afrika.

“Kukua kwa njia za utangazaji za BBC ni ushahidi wa kuwepo kwa mizizi ya muda mrefu na ufahamu wa bara la Afrika. Tunavyoanza safari hii mpya, kwa kweli tuna hamasa kubwa hasa kwa kushirikiana na mashirika ya utangazaji yenye hadhi kubwa katika eneo letu,”alisema Mugera
Uzinduzi huu umekuja muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa kipindi cha TV kwa lugha ya Kiingereza kwa Afrika, Focus on Africa, ambacho pia kinarushwa kupitia Star TV.

Mwezi Julai, siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Olimpiki jijini London, BBC Idhaa ya Ulimwengu ilizindua kipindi kipya cha redio, Newsday – Kipindi ambacho kimelenga zaidi wasikilizaji wa redio wa asubuhi barani Afrika.

Mpaka sasa BBC ina mashabiki 239 milioni kwa wiki duniani kote katika huduma zake za habari za kimataifa ikiwemo BBC World Service, BBC World News TV na bbc.com/news.
BBC Idhaa ya Kiswahili ni sehemu ya BBC Idhaa ya Dunia (BBC World Service), ambao ni watangazaji wa kimataifa wanaotoa huduma ya matangazo kwa lugha mbalimbali kupitia redio, TV na kwenye wavuti na pia kupitia vifaa vitumiavyo visiwaya.

No comments:

Post a Comment

New