My Web

Emmanuel

CONTACT

Friday, August 24, 2012

Rada ya Chenge yaanza kufanya kazi

WAZIRI wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe amesema rada ya kuongozea ndege kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere iliyokuwa imeharibika tangu Agosti 3 mwaka huu, imetengenezwa na  kuanza kufanya kazi juzi saa 2:45 usiku.  Agosti 17 mwaka huu, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilisema rada hiyo iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kutoka Kampuni ya Silaha ya BAE Systems ya Uingereza ilikuwa imeharibika, ikiwa ni siku moja tangu  gazeti dada la Mwananchi (The Citizen) kuripoti  juu ya kuharibika kwa rada hiyo, hali iliyoelezwa kuwa itahatarisha usafiri wa anga nchini.  Alifafanua kwamba kifaa kilichokuwa kinasumbua kimeondolewa na kuwekwa kingine na kuongeza kuwa  wameagiza vifaa vingine vya ziada.

Alifafanua kuwa muundo wa rada upo kama mashine nyingine na kwamba huwa inafanyiwa marekebisho kila mwaka.  Wakati Mwakyembe akieleza hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Fadhili Manongi jana alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akieleza kuwa rada hiyo imetengenezwa baada ya kuwasili kwa kipuri kilichokuwa kimepelekwa  kufanyiwa ukarabati nchini Afrika Kusini na kwamba huduma zimerejea kama kawaida kuanzia jana.

 Dk Mwakyembe alieleza kuwa kila mwaka huwa inasimamishwa kufanya kazi kwa muda fulani ili kufanyiwa ukarabati, kwamba alishangazwa na habari zilizoandikwa kuwa rada ni mbovu.  “Rada kutokufanya kazi kwa siku tano imekuwa habari kubwa kweli hata wenzetu Kenya nao hufanya matengenezo kama sisi” alisema Dk Mwakyembe.

 “Imekuwa kama utaratibu na mwakani  tutasimamisha tena,” alisema Dk Mwakyembe huku akitabasamu na kufafanua zaidi, “Watu wanasema ndege zitaanguka, rada  haiendeshi ndege.”  Alisema kuwa wanaoongoza ndege wamefundishwa njia mbili za kuongoza ndege ambapo njia ya kwanza ni kama rada inafanya kazi na nyingine kama rada inakuwa haifanyi kazi.   “Rada ikiwa nzima basi pale uwanja wa ndege kazi huwa rahisi, ila kama ikiwa mbovu basi kazi huwa mara mbili zaidi ili kuhakikisha kila ndege inafuatiliwa kwa ukaribu,” alisema Dk Mwakyembe.  Huku akitolea mfano wa askari wa usalama barabarani anavyofanya kazi yake kwa shida pale umeme unapokatika, alisema hata rada ikiwa mbovu, ugumu wa kazi huwakumba wafanyakazi wa uwanja wa ndege, “Umeme ukikatika watu si wanaendelea tu kuendesha magari, au siyo”.

  Kutokana na kuharibika kwa kifaa hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Fadhili Manongi alikaririwa akisema Serikali italazimika kutumia Sh400 milioni kwa ajili ya kuagiza kifaa hicho cha mfumo wa kusambaza umeme (Power Supply Unit). 

Rada hiyo ni ile iliyonunuliwa kwa Dola milioni 40 za Marekani na Serikali ya Tanzania kwa Kampuni ya Silaha ya BAE Systems ya Uingereza na ilikuwa haifanyi kazi tangu Agosti 3, mwaka huu baada ya kutokea hitilafu katika kifaa hicho.  Ununuzi wa Rada hiyo ulizua mjadala mkali na kusababisha wabunge  mara kadhaa kuhoji gharama kubwa za ununuzi wake.

Sakata hilo lilimfanya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Clare Short wakati wa Serikali ya Waziri Mkuu Tony Blair, kujiuzulu akipinga Uingereza kuiuzia nchi maskini kama Tanzania rada hiyo kwa bei kubwa.     Kashfa hiyo kwa muda mrefu pia imekuwa ikitajwa kumhusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM).         

No comments:

Post a Comment

New