My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, August 15, 2012

Tuzingatie muda bungeni na sehemu nyingine za kazi

Muda mwingi umekuwa ukipotea bungeni kutokana na baadhi ya mawaziri na wabunge kuanza kuchangia hoja kwa kuongea mambo ambayo kwa kweli hayana msingi wowote kwenye hoja husika. Kwa mfano, unakukuta waziri anaanza kujibu hoja za wabunge waliyochangia makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa kuwataja majina wabunge wote waliochangia wote. Wakati mwingine inamchukua waziri karibu nusu saa akitaja na kushukuru wale wote waliochangia kwenye bajeti yake.

Hotuba nyingine za bajeti zinaanza na utangulizi mrefu ambao hauna uhusiano wowote na bajeti husika. Kwa mfano soma hapo chini utangulizi wa hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2012/2013. Zaidi ya kupoteza muda utangulizi huu hauhusiani kabisa na hotuba ya makadirio ya wizara. Ifike wakati tuzingatie muda hasa bungeni na sehemu nyingine za kazi hasa zile za umma. 

HOTUBA YA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA, MHESHIMIWA SHAMSI VUAI NAHODHA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/2013

UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako Tukufu kupokea taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013.

2. Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kuwasilisha hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka 2012/2013. Pili namshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Nawathibitishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote wa Tanzania kwamba nitatekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.

3. Mheshimiwa Spika, tatu napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri walioteuliwa kushika nyadhifa hizi hivi karibuni. Vile vile nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb.) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge. Nampongeza pia Mhe. Mussa Azan Zungu (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Vile vile napenda kuwapongeza Watanzania waliochaguliwa na Bunge letu Tukufu kuwa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

4. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2011/2012 Wabunge wenzetu watatu waliiaga dunia. Wabunge hao ni Marehemu Jeremia Sumari, Marehemu Mussa Silima na Marehemu Regia Mtema. Napenda kutoa pole za dhati kwako Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, ndugu, marafiki na Watanzania wote kwa ujumla kwa msiba huo mkubwa uliotupata. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao Peponi. Amin.

5. Mheshimiwa Spika, halikadhalika, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli kwa kutupa ushauri na mapendekezo mazuri sana wakati wakichambua mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu. Kamati hii imekuwa ikiishauri vyema Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu njia mbalimbali za kuimarisha utendaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa ili liweze kutekeleza majukumu yake ya Ulinzi wa nchi yetu.

6. Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maelezo yangu kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2012/2013 napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge kuwapongeza Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda (Mb), Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mhe. Dk. William Mgimwa (Mb), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Mheshimiwa Steven Wasira (Mb) kwa hotuba zao ambazo zimetoa mwelekeo katika masuala ya Mipango, Uchumi, Mapato na matumizi ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.

No comments:

Post a Comment

New