My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, November 28, 2011

Kilichotokea Dodoma kwenye vikao vya CCM - Tafsiri yangu

Ndugu zangu
Waafrika sisi tu mahodari sana wa kufunga safari, lakini, huwa hatupangi safari. Kuna tofauti ya kufunga safari na kupanga safari. Kuna tofauti pia ya kuwa na mipango na mikakati na kuwa na mipango na mikakati sahihi.
Mara nyingi wenye kupanga safari zao, na hata kuwa na mipango na mikakati sahihi hufanikiwa zaidi. Na ndivyo ilivyo kwenye siasa.

Kule Dodoma tumeshuhudia ’ Vita vya wenyewe kwa wenyewe’ ndani ya CCM. Inahusu safari ya kuelekea 2015, na si kitu kingine. Kule Dodoma CCM hawakutoka WaMOJA . Wametoka kwenye mapande makubwa mawili na mafungu mengine madogo madogo.

Na CCM ya sasa ina makundi, walau hili wamekiri rasmi CCM wenyewe. Na kwenye kuelekea 2015 tunayaona makundi makubwa mawili; lile linaloongozwa na Edward Lowassa na la akina Samwel Sitta. Kule Dodoma tumeushudia mnyukano wa wazi wa makundi haya yakiwahusisha pia vijana wa chama hicho.

Yote haya yanatoa fursa kwa upinzani kufanya vizuri kama itatumia vema fursa hii ya Wana- CCM wanaonyukana wenyewe kwa wenyewe. Huu ni wakati kwa Wapinzani kuwaonyesha Watanzania kuwa CCM ni chama cha kawaida tu na unaweza kuwepo mbadala wa chama hicho. Ni wakati pia kwa wapinzani kuongeza nguvu ya kusukuma hoja ya kuandikwa Katiba Mpya itakayowashirikisha wananchi katika hatua zote.

Na mpambano ule wa Dodoma, katika hali inayoweza hata kumstajabisha Lowassa mwenyewe, umempa sio tu ushindi Lowassa na kundi lake, bali pia, Lowassa ametoka kwenye vikao vile akiwa, walau kwa wakati huu, na nguvu nyingi zaidi za kisiasa ndani ya chama hicho . Inaonekana ’ jeshi la Lowassa’ ni kubwa, limesambaa na lina nguvu za kimikakati. Ndio, Edward Lowassa amenufaika sana kisiasa na vikao vya chama chake kule Dodoma.

Na mwananchi wa kawaida anasemaje?

Namwuliza , Andrew, kijana dereva wa teksi hapa Iringa; “ Unasemaje kuhusu yaliyotokea Dodoma CCM?”
”Lowassa hayumo!” Ananijibu.
”Una maana gani?” Namwuliza.
”Tuliambiwa Lowassa ni fisadi kumbe hayumo.”

Dereva wa teksi anaonyesha kufurahi kuujua ukweli. Swali ni hili; Je, aliousikia dereva wa teksi ni ukweli kamili? Hivyo basi, waliomwaminisha dereva wa teksi kuwa Lowassa ni fisadi wana mtihani wa kuja na ushahidi wa kumtia hatiani mtuhumiwa ili nao waaminike.

Na katika hili nayakumbuka maandiko ya mwanafasihi Kezilahabi: “ Siku hiyo ikifika utaona ishara itakayokuongoza. Utakapofika pale ambapo kila binadamu lazima afike utajua hukukosea; kwani njia ya kwenda huko inajulikana kwa wote na inakwenda moja kwa moja bila kupinda.

Huna haja ya kusoma kitabu chochote kupata maelezo ya kwenda huko wala hakuna haja ya kusikiliza mahubiri. Hakuna utalaamu unaohitajika maana utajikuta umefika. Utakapofika utamkuta amekaa peke yake akiwatazama wale wengine . Hao wengine utawatambua maana ni ndugu zako wote.

Wengi kati yao ndio wale waliokuwa askari wa mwanga. Wale ambao hutaweza kuwatambua atakumbulisha kwao na wewe utachukua nafasi yako. Usistuke utakaposikia majina yao; maana, wengi kati yao wana majina makubwa. Utawakuta wanafanya jambo fulani. Wewe pia fanya kama wao bila kuuliza bila manung’uniko na usikate tamaa. Kwa sasa hivi subiri ishara” ( E. Kezilahabi, Nagona)

Ni kina nani wamejeruhiwa Dodoma?

Nape Nnauye hawezi kuwa mwana- CCM mwenye furaha kwa wakati huu. Nahofia kuna hesabu za kisiasa alizozichanganya vibaya sana. Kama mwenezi wa chama alijichanganya sana kwenye kuilezea kwa umma dhana ya ’ Kujivua Gamba’ . Badala ya kuonekan kuwa ni mkakati wa mabadiliko ya jumla kwa CCM Nape aliitumia dhana hiyo kuwahukumu WanaCCM wenzake . Hivyo basi, kuonekana zaidi kuwa ni mbinu ya kutaka kuondokana nao ili kupisha njia kwa watu wa kundi lake. Na hapo ndio kwenye tatizo la msingi kwa Nape. Kwamba anaonekana kuwa na kundi lake kuelekea 2015.

Kujichanganya kwa Nape kimsingi kumewapa fursa akina Lowassa na wenzake kupanga mashambulizi na kuyatekeleza kwa mafanikio makubwa. Na kama kuna mtu aliyejeruhiwa vibaya kwenye vikao vya Dodoma ni Nape Moses Nnauye. Ana lazima ya kujipanga na kurudisha mashambulizi ili kulinda heshima yake na hata taswira yake kwa jamii. Hivyo hivyo kwa Samwel Sitta na wenzake. Dakika 45 za kuongea peke yake kwenye ITV hazikumwongezea nguvu Samwel Sitta na kundi lake na labda kinyume chake.

Je, ina maana vita ndani ya CCM ndio imekoma?
Hapana, huu ni mwanzo tu, vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM vitaendelea na moto wake kuongezeka. Mwakani kuna uchaguzi wa ndani ya chama hicho. Tulichokiona Dodoma ni ’ rasha-rasha’ tu. Kutoka Dodoma makundi yanayohasiamiana ndani ya CCM yatazidi kupambana mikoani, wilayani na hata kwenye kata. Watazidi kupambana pia kupitia vyombo vya habari. Yote ni katika kuhakikisha wanajipanga kushika nafasi muhimu kwenye uchaguzi ujao wa chama chao, nafasi zitakazohakikisha wagombea wao wanapata tiketi za kuwania urais na hatimaye kushika dola.

Na Lowassa na wenzake wana kibarua kigumu cha kuwabadilisha WaTanzania kutoka kile walichoaminishwa kabla . Ni kibarua kigumu kama vile kumwambia mtu kuwa rangi nyekundu si nyekundu tena bali ni nyeupe. Kwamba alichokuwa akiamini mtu huyo siku zote kuwa ndicho, sicho. Ni watu hawa hawa ambao hawakupata tabu jana kujibu swali la je, fisadi mkuu ni nani? Na anayefuatia….?

Je, uchaguzi wa ndani ya CCM ukimalizika mwakani ndio mwisho wa vita?

Hapana, kundi litakaloibuka na ushindi wa jumla litahamishia mapambano yake kwa wapinzani wa chama na mgombea wao Urais walio nje ya chama chao. Kwa ilivyo sasa mashambuzi yanaweza kuelekea kwa Chadema. Hiki ni chama chenye nguvu na ushawishi mkubwa kwa wananchi kwa sasa.

Hivi ni Lowassa tu aliyeibuka mshindi kule Dodoma?
Hapana, kuna MwanaCCM mwingine aliyetoka Dodoma kimya kimya huku kikapu chake kikiwa kimejaa mavuno. Ni Fredrick Tluway Sumaye. Msomaji lishike jina hili. Huyu bwana hadi wakati huu anazicheza karata zake vizuri sana. Yaelekea mafunzo yake ya Uongozi aliyoyapata kule Havard Marekani yanamsaidia.
Si tulimsikia Sumaye kule Dodoma akisimama na kumtetea ’ majeruhi’ mwenzake Lowassa bila kutamka kuwa naye, Sumaye ni ’ majeruhi’ wa ’ Siasa uchwara’ kama anavyoziita Rostam Aziz. Sumaye ana mitaji ya kisiasa anayowekeza.

Je, ni kweli Lowassa ana nguvu na ushawishi mkubwa kisiasa?

Nikijibu hapana nitaongopa. Edward Lowassa ni mwanasiasa mahiri na mwenye ushawishi mkubwa ndani na hata nje ya chama chake. Wanaomjua Lowassa wanasema ana vitu viwili vikubwa; authority na humbleness. Kwamba ana uwezo wa kushawishi na kufanya vitu vifanyike na pia ni mnyenyekevu. Hilo la mwisho kuna wanaosema Lowassa anaweza kuongea na mtu mdogo sana, lakini atahakikisha hajibu simu ya mtu mwingine mpaka amalize mazungumzo na anayeongea nae.

Nikiwa Bagamoyo kwenye mkutano wa masuala ya elimu juma la jana kuna hoja ilizuka juu ya shule za sekondari za kata. Kikundi cha majadiliano nilichokuwamo kiliwajumuisha watendaji wa elimu kutoka Wilaya mbali mbali za Tanzania.
Swali likaulizwa; ” Ilikuaje sekondari za kata zikajengwa kwa kasi vile?”
”Ni Lowassa!” Alijibu mmoja wa washiriki.

Alifanyaje? Akauliza mwingine.
”Waliokuwa wakiratibu michango ya elfu kumi kumi kutoka kwa Watumishi walitwambia; Lowassa anataka tumpelekee orodha ya ambao hawakulipa michango hiyo, si orodha ya waliyolipa. Ni kwa njia hiyo kila mmoja wetu akachangia na shule zikajengwa. Ni nani anayetaka jina lake lifikishwe kwa Lowassa?” Alimalizia kwa kuuliza mmoja wa wanakikundi cha majadiliano.

Na kwa yaliyotokea Dodoma kuna watakaoshika tama na kusema, kumbe, Edward Lowassa hajamalizwa kisiasa! Je, akina Mwakyembe hawakufahamu, kuwa simba humwui kwa risasi ya kumpapasa masikioni?
Kama ni mchezo wa ngumi, basi, kwa mpinzani wa Lowassa, akubali, kuwa kummaliza Lowassa , awe tayari kucheza raundi zote 12.

Naam, tutayaona mengi mengine huko twendako, tuombe uhai.

No comments:

Post a Comment

New