My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, November 2, 2011

UNAISHI MBALI NA MPENZI WAKO - 2

WAPENZI kuishi mbalimbali ni mtihani mkubwa. Wengi hujawa na hofu, wanahisi watasalitiwa na kupoteza matumaini ya uhai wa penzi lao. Inawezekana kuna ukweli wa jambo hilo, lakini hapa katika All About Love ipo dawa ya kukuondolea wasiwasi.

Yes! Unaweza kuwa mbali na mpenzi wako lakini ukawa kama unaishi naye jirani kabisa; yeye Tandika, wewe Kimara! Ni kama vile wewe uko Raskazone, yeye Sahare (Tanga) au uko Mbauda, yeye Kwa Ngulelo (Arusha). Jirani kabisa.
Njia ya kwanza niliyobainisha wiki iliyopita ilikuwa ni mawasiliano. Kwa kuanzia nilifafanua namna ya kumsogeza mpenzi wako kwa kutumia barua pepe na simu, leo tunaendeela na aina nyingine ya mawasiliano. Karibuni darasani.

(iii) Barua
Hii siyo njia nzuri sana hasa kwa nyakati hizi za kupanuka kwa utandawazi. Ni njia ambayo huchelewesha ujumbe kufika, na pengine ni kama imepoteza ladha. Hata hivyo, mwenzi wako anaweza akawa yupo mbali kikazi, sehemu ambayo haina mawasiliano ya simu au waraka pepe, unaweza kulazimika kutumia njia hii.

Inawezekana yupo katika sehemu ambayo huduma zote zinapatikana lakini unaweza kumtumia barua ikiwa ni njia ya kumfurahisha au kumchekesha! Unampigia simu kama kawaida, unamwandikia waraka pepe kama kawaida lakini bado unamtumia barua, tena lazima uwe umeandika kwa mkono wako mwenyewe, ukionyesha jinsi unavyompenda.

Itakuwa vizuri zaidi kama ukimwandikia kwa mtindo wa mashairi na hata kama hujui, unaweza kutumia wataalamu wa mashairi au meseji za mapenzi ambao watakusaidia kukuandikia tungo nzuri za kimapenzi zitakazomfanya mpenzi wako afurahie kuwa na wewe.

Katika barua yako ni vizuri kama utapulizia manukato unayopenda kuyatumia, hii itamfanya asikie harufu yako japo utakuwa upo mbali naye.

(iv) Kadi
Hii nayo ni kati ya njia bora ambazo zitakuweka karibu zaidi na mpenzi wako. Chagua kadi nzuri sana, ambayo ina ujumbe mwanana, ukieleza jinsi unavyompenda kwa dhati ya moyo wako.

Ni vizuri pia kama ukieleza jinsi unavyomuonea wivu kwa yeye kuwa mbali na wewe. Eleza mapenzi yako, kwa njia ya ujumbe uliopo kwenye kadi, lakini pia andika ujumbe wako kwa mkono wako mwenyewe sehemu ambayo haina maandishi.
Usimtumie kadi kila wakati, mtumie mara chache sana, tena kwa kumshtukiza.

Kwa kufanya hivi, bado utakuwa umejisogeza karibu zaidi na mpenzi wako. Inashauriwa kumtumia kadi mpenzi wako si zaidi ya mara moja kwa mwezi. Njia hii itamfanya mwenzi wako aone thamani yako na jinsi ambavyo unampenda hata akiwa mbali na wewe.

ZAWADI
Kumtumia mwenzi wako zawadi ni kati ya mambo ambayo humfanya mpenzi wako afurahie uhusiano wake na wewe. Hakuna zawadi za moja kwa moja ambazo ni rasmi kwa ajili ya mwenzi wako, lakini ni vyema ukamtumia zawadi kulingana na mapenzi yake zaidi.

Kwa kuwa wewe unamfahamu zaidi mwenzi wako, unaweza kujua zawadi gani ni nzuri kwake au anayopendelea zaidi kuliko aina nyingine. Katika vipengele vifuatavyo, nimechambua aina kuu za zawadi ambazo ukimtumia mpenzi wako unamteka hisia zake na kuona kana kwamba yupo karibu na wewe hata kama yupo mbali.

(i) Mavazi
Mavazi ni kati ya zawadi ambazo zitamfanya mpenzi wako azidi kukupenda na kuwa karibu zaidi na wewe. Kama nilivyotangulia kusema awali, aina ya nguo ambazo unaweza kumtumia mpenzi wako ni zile ambazo unadhani atavutiwa nazo zaidi au zile ambazo zitampendeza na kumfanya aonekane nadhifu.

Hata hivyo, zipo aina za mavazi ambazo zimependekezwa zaidi kwa ajili ya wenzi kutumiana wanapokuwa mbali.
KWA WANAUME: Kama wewe ni mwanamke unataka kumtumia mwezi wako wa kiume, mavazi haya yanafaa zaidi. Saa nzuri ya mkononi, nguo za ndani, lakini lazima uzingatie rangi ya bluu, bluu bahari au nyeupe kimsingi zisiwe za rangi inayoficha uchafu.

Zingine ni fulana za ndani, T. Shirt, mkanda wa kiunoni, simu ya mkononi, vitambaa vya jasho n.k. hakikisha katika zawadi zako hizo, unaambatanisha na manukato mazuri (hasa unayotumia wewe).

Haishauriwi kumtumia suruali au shati kwa sababu inaweza kuwa kubwa au ndogo, hivyo kupunguza ladha ya zawadi hasa kama atakuwa ameipenda. Zawadi za aina hiyo, unaweza kumpa mwenzi wako ofa ya kwenda kuchagua moja kwa moja dukani.

KWA WANAWAKE: Kama wewe ni mwanaume na unataka kumtumia mpenzi wako wa kike zawadi, lazima uwe makini sana! Mavazi yaliyopendekezwa hapa ni pamoja na batiki (gauni, blauzi na sketi, blauzi yenyewe n.k), hereni, bangili, mkufu wa vito, simu ya mkononi, saa ya mkononi, nguo za ndani (kulingana na mapendekezo yake, kwa jinsi umjuavyo), sidiria, viatu n.k.

Kama umesoma vizuri utaona mwanamke anaweza kununuliwa vitu vingi zaidi (hasa nguo) tofauti na mwanaume. Hii inatokana na aina za mavazi na saizi zao kukaririka kirahisi zaidi au kutokuwa na saizi ya moja kwa moja.
Mathalani, batiki, sketi na blauzi na vinginevyo. Kama kawaida, mavazi haya, ambatanisha na manukato mazuri, hasa yale ambayo unapenda kutumia wewe.

Bado kuna aina nyingine ya zawadi ambazo unatakiwa kumtumia mpenzi wako na kumfanya awe karibu zaidi na wewe kihisia na hivyo kuzima kabisa hisia za kukusaliti. Pia, kuna vipengele vingine ambavyo ni dawa ya hofu kwa mwenzi anayeishi mbali nawe.

ladha. Hata hivyo, mwenzi wako…

No comments:

Post a Comment

New