My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, November 1, 2011

Kulazimisha penzi lililokufa ni kujitakia aibu, Mateso

KILA mtu anapenda kwa maana ya yule ambaye nafsi yake imemdondokea. Lakini haijawahi kusemwa kwamba mapenzi ni utumwa.

Inawezekana ukawa hujapata mantiki ya hoja yangu hapo. Labda nikufafanulie kuwa tatizo linalowakabili watu wengi ni kushindwa kusoma alama za nyakati.

Namaanisha kutokufahamu kipimo cha mapenzi na wakati wake. Inawezekana alikupenda na unampenda lakini mabadiliko yake yakupe picha ili ujue cha kufanya.

Unangoja akuoneshe mpenzi mwingine ndiyo ujue kuwa zama zako zimefika tamati? Akufukuze kama mbwa na matusi juu? Usingoje aibu, heri nusu shari kuliko shari kamili.

Mwanafasihi wa Kimanzichana, Abbas Hamis Kinzasa ‘20%’ katika wimbo “Ya Nini Malumbano” anaimba: “Najiweka pembeni kuepusha msongamano.” Hebu na wewe kaa pembeni kwa hiari yako.

Thamani yako ni kubwa mara sabini kama utakuwa mwelewa na kujiondoa kuliko taadhira ya kutupiwa virago. Kuna penzi hai na lililokufa, weka akilini na uheshimu.

SOMA MFANO HUU
Ester alifunga ndoa na Sam miaka minne iliyopita. Walielewana vema siku za mwanzo za uhusiano wao. Wakapata mtoto mmoja ambaye naomba nisimtaje jina kwa sababu hii kesi haimhusu.

Uhusiano wao ulidumu miaka miwili tu, kwa hiyo kuna zaidi ya miaka miwili mingine tangu walipoachana. Kila mtu anaendelea na maisha yake lakini ipo wazi kwamba Ester hajakubali matokeo.

Sam anaendelea kutoa matumizi kama kawaida kumhudumia mtoto. Hii ina maana kwamba suala la matumizi siyo mgogoro kabisa baina ya wanandoa hao walioamua kuachana.

Hata hivyo, baada ya kuachana, mwaka mmoja baadaye Sam alioa mke mwingine. Hapo ndipo mtafaruku unapoanzia. Ester hataki kukubali kwamba mume wake wa zamani sasa ni mali ya mwingine.

Kila siku visa. Mbaya zaidi anaviendesha mpaka kwenye hatua ya kuropoka ovyo. Watu wanaomsikiliza wanamdharau. Wanamwona hamnazo. Angeweza kuepuka aibu hiyo kama angetambua kwamba penzi limeshakufa.

VISA VYA ESTER
Miezi miwili iliyopita, Sam alipata matatizo ya polisi, akawekwa mahabusu. Eti hilo likawa la faida kwa Ester, kwani alitangaza kila kona kwamba mume wake wa zamani ameoa mwanamke mwenye gundu.

Kwamba mke wa sasa wa Sam ana gundu ndiyo maana amepata matatizo ya polisi. Ester alishindwa kutambua kwamba huyo mwanaume amezaa naye, kwa hiyo wanashirikiana kulea.

Siku ya siku Ester kafunga safari mpaka kwa wakwe. Huko akatema cheche. Matusi ukweni. Sam kwa hasira ikabidi amfukuze kwa maneno makali “Sikutaki”. Ikawa faida mtaani, majirani wambeya vicheko, sinema ya bure.

UKWELI NI HUU
Kinachomtesa Ester si kingine, bali mapenzi. Anataka aendelee kummiliki Sam wakati kwa sasa yupo kwenye himaya ya mwingine. Mapenzi ni kama kiti cha basi, ukishuka, anakaa mwingine.

Sina maana kuwa watu waachane mara kwa mara la hasha! Nasimamia ukweli kuwa inapolazimu kuachana, basi inua mikono bila kinyongo. Fikiria wako anayekuja, ya nyuma sahau.

Unaweza kuona aibu ambayo Ester aliipata baada ya kutimuliwa kwa matusi na Sam huku akimsindikiza kwa neno “sikutaki” ambalo alilipaza kwa juu na kila shuhuda alilisikia. Tena alilirudia mara kwa mara.

TAHADHARI
Kwa nini uambiwe “toka”, “sikutaki” na mengineyo yenye kukuaibisha na kutesa moyo wako? Unapaswa kusoma alama. Ujue kipimo cha mapenzi yenu ili uwe na pakushikia.

No comments:

Post a Comment

New