My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, January 23, 2012

GLOBAL Sindano 11 zitakazotibu tabia yako ya wivu - 2

KATIKA kipengele “Ongeza Uaminifu” ambacho nilimaliza nacho wiki iliyopita, nilieleza kwamba mojawapo ya dawa nzuri ya kukabiliana na wivu ni kuongeza kiwango cha uaminifu.
Muamini mwenzi wako na utaona jinsi mambo yatakavyokwenda. Tunza akilini kwamba kutengeneza uhusiano imara na wenye mafanikio, huhitaji kiwango kikubwa cha uaminifu.
Amini kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo. Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda ‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.
Kwa kawaida, anaweza kuwepo mtu ambaye atakufanya usimuamini mwenzi wako hata kidogo. Inawezekana akakujengea picha kutokana na maneno ya zamani au matukio yaliyopita. Je, unaona wivu kwa sababu umeambiwa mpenzi wako aliwahi kutoka na watu wawili tofauti kabla yako?
Wivu wa nini? Kwa nini maneno hayo yakuchanganye akili? Je, ulimkuta akiwa mbumbumbu wa mapenzi na hajawahi kutoka na yeyote? Kumbe utabaini kuwa historia ya mwenzi wako haina maana inayokubalika kwenye uhusiano endelevu.
Wanasema shetani wa jana, leo anaweza kuwa malaika. Vilevile malaika wa leo kesho anaweza kuwa shetani. Inawezekana hao ulioambiwa alitoka nao walimtenda ndiyo maana hakuwapa nafasi ya kudumu lakini wewe umepata fursa hiyo kwa sababu unakidhi mahitaji yake. Hata hivyo, hii haina maana kuwa kila wivu unaotokana na kuambiwa hauna maana. Yapo mengi yenye maana.

8. MWONESHE MWENZI WAKO
Ukiwa na mwenzi wako, muoneshe kwa mifano halisi jinsi unavyojisikia au unavyoweza kumtendea katika nyakati ambazo unamuonea wivu. Kufanya hivyo, ni rahisi kwako kutambua maumivu yako, vilevile na yeye atajua mahali ambako anakosa mengi matamu.
Mtu anapoona wivu wa ndani, husumbuliwa na maumivu ya moyo. Aghalabu, akili yake hushindwa kufanya kazi inavyotakiwa. Mantiki ya hoja hiyo ni kwamba mwenzi wako hawezi kukutendea mambo matamu, ikiwa kichwa chake hakitakuwa katika hali ya kawaida.
Unaweza pia kuvuta picha na kujadili muonekano wako pindi unapokuwa na wivu. Hakikisha mwenzi wako anakuelewa kinaga ubaga kile unachomaanisha. Je, umegundua umepoteza raha kiasi gani? Umefahamu namna ambavyo huwa unaboa? Mpe uhuru mpenzi wako akwambie ukweli.
Inawezekana akawa anasita kukwambia bayana kutokana na hofu. Unapaswa kulijua hilo mapema. Unaweza kumpa nafasi aseme, akakujibu hakuna kitu. Ukishagundua kuwa anakohofia, jaribu kumshawishi ili afunguke. Akikubali kueleza la moyoni, ni tiba kubwa kwako.
Bila shaka utagundua ni kiasi gani anakerwa na tabia yako ya wivu. Je, ni nani anapenda kumuudhi mwenzi wake kila siku? Hakuna na kwa hakika hata wewe mwenyewe hupendi. Hivyo basi, amani yake itatokana na tabia yako ya kumuonea wivu.
Fikiria kuwa anashindwa kuwa mtulivu kufanya jambo lolote kwa sababu anahofu unaweza kulipokea tofauti. Kwa nini unamnyima uhuru kwa sababu ya wivu wako? Fungua moyo leo, muoneshe kuwa unamuamini. Imani yako itamfanya aongeze upendo kwako. Siku zote, mapenzi husafiri kwa mtindo wa nipe nikupe.
Hata hivyo, njia hii kwa watu wengine hushindwa kufanya kazi. Inapasa mtu mwenyewe awe amedhamiria kurejesha amani na furaha kwake na kwa mwenzi wake. Vema uzingatie kwamba wivu ukizidi ni ushamba. Jamii itakudharau, hata mwenzi wako akikuchoka, anaweza kukugeuza zuzu.

7. JIAMINI
Wivu mara nyingi huanza kutokana na kukosa kujiamini. Jiulize, unajisikia salama wewe mwenyewe? Je, unaogopa kwamba mpenzi wako anaweza kukuacha kwa sababu umepungukiwa sifa kadhaa? Mambo mengi kati ya hayo yanapogota kichwani, huyafanya maisha yako yatawaliwe na wivu.
Inawezekana mwenzi wako anakupenda kuliko wewe unavyompenda. Si ajabu, akawa anawaza kufanya maisha bora zaidi akiwa na wewe. Amekukubali kwa namna ulivyo kiasi kwamba hawazi kukupoteza. Tofauti na mawazo yake, tabia yako ya kutojiamini, hufikiria kwamba hakupendi.

No comments:

Post a Comment

New