My Web

Emmanuel

CONTACT

Saturday, June 23, 2012

Kuelekea Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Ulimwenguni



Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ndio chombo kilichopewa jukumu la kuratibu masuala yote yanayohusu dawa haramu za kulevya hapa nchini kupitia mikakati yake mikuu miwili ya kuzuia matumizi  na ule wa kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya. 

Ikumbukwe kwamba biashara ya dawa za kulevya ndio huchochea matumizi ya dawa hizo na kuleta athari kwa mustakabali wa Taifa letu kiafya, kijamii, kiuchumi, kisiasa na hata kimazingira.

 Tume ikishirikiana na vyombo vya dola hususani Kikosi kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya imeshuhudia ongezeko la biashara hiyo haramu kutokana na  kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kinachokamatwa. Mfano; Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2011 kilo 264.3 za dawa ya kulevya aina ya heroin zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka 2010 ikiwa ni ongezeko la 42% la kiasi cha heroin kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu. 

mtumia madawa ya kulevya
Aidha, mwaka 2011 kilo 126 za dawa ya kulevya aina ya cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa mwaka 2010, ambalo ni ongezeko la 100%. Ongezeko hili kubwa la ukamataji linaashiria kukua kwa biashara haramu ya dawa za kulevya kunakorahisisha upatikanaji wa dawa hizo na kuchangia kuongezeka kwa idadi ya watumiaji nchini.

Ingawa hakuna takwimu sahihi za watumiaji wa dawa za kulevya nchini, inakadiriwa takribani watu 150,000 hadi 500,000 wanatumia dawa hizo. Aidha, ingawa sehemu ndogo tu ya watumiaji wa dawa za kulevya hufika katika vituo vya afya kwa minajili ya kutafuta tiba kumekuwa na ongezeko mahitaji ya tiba katika vituo mbalimbali vya afya. 

Hali hii inazidi kudhihirisha kuwa pamoja na ongezeko la biashara ya dawa za kulevya matumizi ya dawa hizi nayo yameongezeka. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2011 jumla ya watumiaji 4,684 wa dawa za kulevya walihudumiwa katika vituo vya afya vya manispaa na majiji nchini.

 Halikadhalika, takwimu kutoka hospitali ya Mirembe zilionyesha ongezeko la vijana waathirika wa dawa za kulevya kutoka 290 mwaka 2000 hadi kufikia 569 mwaka 2005 sawa na nyongeza ya 96.2%. Katika kukabilina na hali hii serikali ya Tanzania ilishirikiana na ile ya Marekani ilianzisha tiba ya majaribio kwa wanaojidunga heroin kwa kutumia dawa ya methadone mwezi Mei, 2011 ili kuwapunguzia hatari ya maambukizi ya VVU miongoni mwao. 

Hadi kufikia mwezi Desemba 2011 wajidunga heroin wapatao 250 walikuwa wakipata tiba hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Matumizi na biashara ya dawa za kulevya huleta huathiri jamii husika kwa namna mbalimbali ikiwemo kiafya, kiuchumi na kisiasa. Athari za kiafya huhusisha uwezekano wa kupata maradhi ya moyo, ini, mapafu, meno, figo, tumbo, ngozi, maradhi ya akili, kansa, ugumba, kuzaa watoto wafu, utegemezi, uteja, kusababisha au kupata ajali na hata vifo. 

Aidha, matumizi ya dawa za kulevya huchochea maambukizi ya VVU kutokana na kushirikiana sindano kwa wale wanaojidunga na kufanya ngono zisizo salama. Kwa wale waliokwisha ambukizwa VVU wanapoendelea kutumia dawa za kulevya kinga yao hushuka haraka zaidi ya wale wasiotumia dawa hizi na kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa nyemelezi kama vile homa ya ini, kifua kikuu, kaswende na kisonono. 

Katika utafiti uliofanyika mkoani Dar es Salaam mwaka 2006 ulionyesha kuwa 42% ya wajidunga walikuwa wamepata maambukizi ya VVU. Utafiti mwingine uliofanyika kwa wajidunga wilayani Temeke mwaka 2010 na Asasi ya Medicins Du Monde uligundua 34.8% ya wanaojidunga heroin waligundulika na VVU na wengine 27.7% waligundulika na virusi vya homa ya ini.

Kiuchumi, matumizi ya dawa za kulevya ambayo huathiri zaidi vijana ambao ndio nguvukazi ya Taifa hurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa kuongeza wategemezi hivyo kupunguza uzalishaji. Vilevile, serikali inaongezewa mzigo kwa kutumia rasilimali ambazo zingeweza kutumika katika sekta nyingine za maendeleo katika kukabilina na tatizo hili. 

Biashara na matumizi ya dawa za kulevya huvuruga mfumo wa maisha katika jamii ikiwa ni pamoja na kumomonyoka kwa maadili ikiwemo biashara ya ngono, kudharaulika kwa tamaduni za jamii, rushwa, kushuka kwa kiwango cha elimu, utoro mashuleni na kazini na migogoro ya kifamilia ambayo inachangia kuvunjika kwa ndoa na ongezeko la watoto wa mitaani. 

Kwa upande wa kisiasa, biashara ya dawa za kulevya huweza kusababisha kuchaguliwa kwa viongozi wanaofanya biashara hiyo hivyo kudhoofisha jitihada za serikali za kudhibiti  biashara haramu ya dawa za kulevya. Aidha, watumiaji wanaweza kurubuniwa kirahisi kuchagua wanasiasa wanaojihusisha na biashara hiyo haramu. 

Kiusalama, matumizi na biashara ya dawa za kulevya huhatarisha usalama katika jamii kwa kuongeza uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na ongezeko la vitendo vya wizi, utapeli, uporaji, ubakaji na ajali za barabarani. 

Biashara ya dawa za kulevya pia huweza kuongeza matukio ya ugaidi, utekaji nyara, vita vya wenyewe kwa wenyewe au vita kati ya serikali na magenge ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kama inavyotokea hivi sasa katika nchi ya Mexico. Vilevile, kuna hatari ya uharibifu wa misitu na kukauka kwa vyanzo vya maji iwapo kilimo cha dawa hizi utafanyika kwenye misitu au kwenye vyanzo vya maji. 

Mafanikio

Pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume pamoja na wadau wake imeweza kufanikisha mambo yafuatayo:-
(i)        Kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha  dawa za kulevya za heroin na cocaine
(ii)      Elimu ya dawa za kulevya imeweza kufikia watu wengi zaidi ikiwemo waumini wa dini mbalimbali kupitia viongozi wao;
(iii)    Kukua kwa ushirikiano kati ya vyombo vya dola na Kikosi Kazi kulikosaidia kupambana na biashara ya dawa za kulevya
(iv)    Uanzishaji wa Huduma ya tiba ya majaribio kwa wajidunga wa heroin kwa kutumia dawa ya methadone
(v)      Kuanzishwa kwa baraza la viongozi wa dini kwa ajili ya kuwahamasisha waumini wao kushiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Changamoto

(i)   Kuendelea kuwepo kwa unyanyapaa katika jamii dhidi ya watumiaji wa dawa za kulevya kunawakosesha fursa ya kupata tiba.
(ii)  Uelewa mdogo wa masuala ya dawa za kulevya huifanya jamii ione kama  uraibu wa dawa za kulevya ni jambo la kujitakia na si ugonjwa;
(iii) Kushamiri kwa kilimo cha bangi nchini;
(iv) Kuwepo kwa mipaka mingi, ukanda mrefu wa pwani (bahari na maziwa), vipenyo vingi na njia zisizo rasmi katika mipaka ya nchi yetu hali inayorahisisha biashara ya dawa za kulevya;

Mikakati ya Baadaye

(i)           Kuanzisha huduma za makazi ya kupata nafuu (sober houses) kwa watumiaji dawa za kulevya Tanzania bara;
(ii)         Kuendelea kuhamasisha watumiaji wa dawa za kulevya na waliopata nafuu kuhudhuria mikutano ya kuacha na kutorudia matumizi ya dawa za kulevya (Narcotic Anonymous -NA);
(iii)       Kuendelea kutoa elimu kwa umma kwenye matukio maalum ya kitaifa,  semina, makongamano, luninga, redio na machapisho;
(iv)       Kuwawezesha vijana wanaoacha kutumia dawa za kulevya kwa kuwapa stadi za maisha ili waweze kujitegemea;
(v)         Kupanua huduma za kupunguza maambukizi ya VVU miongoni mwa watumiaji;
(vi)       Kuweka sera ya Taifa, kurekebisha sheria na muundo wa chombo cha kudhibiti dawa za kulevya.

Aidha, Tume inaukaribisha umma wa Tanzania kuadhimisha Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Ulimwenguni ambayo huadhimishwa tarehe 26 Juni ya kila mwaka ikiwa ni ishara ya kuungana na mataifa mengine duniani yaliyo kwenye harakati za kupambana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. 

Mwaka huu maadhimisho haya ya kitaifa yatafanyika Mkoani Dar es Salaam, Wilaya ya Kinondoni kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Tandale. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni“Tujenge Jamii yenye Afya bila Dawa za Kulevya: Tutoe maoni ya Katiba na Kushiriki sensa ya mwaka 2012

No comments:

Post a Comment

New