My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, June 19, 2012

WABUNGE: BAJETI IMEONGEZA MZIGO KWA WANANCHI

KWANZA tumuombe Mungu azidi kuifanya nchi yetu kuwa ya amani na mshikamano na awageuze akili wale wote wenye mawazo ya kuifanya nchi hii kuwa na vita, awatie mawazo ya kushikamana na kukemea wale wote wanaofuja mali za umma kwa manufaa yao, aijaze nchi baraka ili tuishi kwa furaha na wale wote wenye nia ya kuhujumu uchumi wa nchi awaumbue, waaibike mbele ya jamii.
Baada ya kusema hayo leo nitakuwa nazungumzia Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/2013 iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, niseme wazi kwamba imeongeza mzigo kwa walipa kodi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa serikali.
Kiukweli nilipoisikiliza bajeti hiyo nimegundua kuwa hakuna matumaini kwa Watanzania wa kawaida kwani fedha nyingi zimerundikwa kuwanufaisha wachache huku umma ukiambulia patupu.
Katika bajeti hiyo hakuna mkataba wa makusudi wa kupunguza matumizi ya serikali, ahadi yake ya kupunguza matumizi kwa kupunguza posho zisizo na tija na matumizi mengine haikutekelezwa. Nimeshangazwa na kutokuwapo kwa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma na badala yake fedha nyingi kurundikwa katika matumizi ya kawaida ya serikali.

Mfumo wa kodi kama mlivyosikia ni mbaya kabisa, hakuna kinachoashiria kwamba mkulima wa kawaida atapunguziwa mzigo na badala yake serikali inaendelea kuwanufaisha wafanyabiashara wa vyakula kwa kuwaruhusu kuagiza vyakula nje bila kodi, hiki naweza kusema ni hatari kwa soko la mazao ya wakulima wetu hapa nchini.
Ki ukweli hakuna ubunifu kwenye kupanua wigo wa kodi, tungeweza kusikia katika construction (sekta ya ujenzi) ambayo inakua haraka na inachukua asilimia 18 ya pato la taifa kwamba tungetoza kodi huko, lakini badala yake ni yaleyale ya siku zote, kodi kwenye sigara, vinywaji na bia.
Ninachoona mimi ni kwamba matatizo makubwa katika bajeti hiyo ni kutengwa kwa fedha kidogo za maendeleo na kwamba kinachoshangaza ni serikali kushindwa hata kugharamia matumizi ya kawaida.
Utawala unagharamiwa kwa shilingi trilioni 10 hali uwezo wa kukusanya mapato ya ndani ni shilingi trilioni 8, hii inamaanisha kwamba serikali yetu pia inatumia fedha za wahisani kugharamia matumizi ya kawaida, kitu ambacho ni hatari kwani wafadhili wanaweza wasitoe fedha kwa sababu zozote zile.
Iko haja kwa serikali kujifunza kubadilika kwani kilichotangazwa wiki iliyopita kwenye bajeti yake ni marudio ya miaka yote. Huwezi kuchukua fedha zote ukaurundikia utawala halafu ukawaacha wananchi bila kitu, hicho ndicho tulichokiona wiki iliyopita na ambacho nimeona niwashauri wabunge wakiangalie kwa umakini.
Waziri wa Fedha, Dk. Mgimwa ametangaza kuwa shilingi trilioni 10 ni kwa ajili ya mishahara na watumishi na matumizi ya kawaida, maendeleo ambako ndiko wananchi wa kawaida waliko kumeachwa tena kutegemea fedha za wafadhili.
Kinachoshangaza wengi ni kuwa mwaka jana serikali ilikuja na bajeti kama hii ya kutegemea fedha za wafadhili, zaidi ya asilimia 40 ya fedha zilizotengwa hazikupatikana na leo wanakuja na bajeti ya aina ileile, hii ni hatari.
Kwa upande mwingine bajeti hii ni pigo kubwa kwa wafugaji kwani wameshindwa kutengewa fedha kwa ajili ya kuboresha ufugaji hasa wale ambao wanahamahama kwani wizara husika imepunguziwa fedha.
Lakini siyo kwamba bajeti yote ni mbaya, hapana, naipongeza katika kipengele cha uboreshaji wa reli ya kati, serikali imefanya vyema kwa kutenga fedha hizo.
Bajeti hii kama nilivyoisikiliza kiukweli imeendelea kukosa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na hivyo kuongeza makusanyo ya ndani matokeo yake ni kwamba fedha zilizotengwa kwenye Wizara ya Elimu ni ndogo kiasi cha kutoweza kukidhi mahitaji ya walimu na na natabiri kuwa fedha zilizotengwa zitaendeleza migogoro.
Sijui kama walifikiria kwa kina upandishaji wa gharama za simu maana haiwezekani kodi ya huduma ya simu ikapandishwa na kulingana na nchi za Afrika Mashariki bila kujali kwamba itawaumiza watumiaji wa hali ya chini.
Bajeti hii haina kipaumbele kwa huduma za kijamii na imejikita kwenye masuala ya anasa na kifupi ni kwamba haina tofauti na zilizowahi kutolewa. Nilitegemea kwa kuwa bajeti ya mwaka jana haikuwa na ufanisi, mwaka huu ningesikia maelezo ya kina yakifafanua sababu za kutofanya vizuri kwa bajeti ya mwaka jana, jambo ambalo halikufanyika.
Hata ongezeko la shilingi trilioni mbili kwa Bajeti ya 2012/13 ikilinganishwa na iliyopita, siyo jambo geni kwani limekuwa likifanyika mara kadhaa lakini ufanisi wake hauonekani.
Kutokana na haya niliyoyabaini naamini sasa kazi ni kwenu wabunge ambao mtapewa nafasi ya kuichambua kwa niaba ya sisi ambao tupo nje ya bunge. Huduma za simu, huduma za jamii na zile za maendeleo ni lazima mzijadili na kuona kama kutakuwa na marekebisho la sivyo itakuwa haina jipya na itajaa maumivu kwa walalahoi. Ni changamoto kwa wabunge wote bila kujali itikadi za kisiasa.

No comments:

Post a Comment

New