My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, June 19, 2012

LISHE NDIYO KILA KITU


Kaka.

Samaki.


Karanga.
KATIKA makala zetu zilizopita, tuliwahi kuandika kuhusu dhana nzima ya Ukimwi na kusema kuwa Ukimwi siyo ugonjwa bali ni hali.
Tulifafanua kuwa maana ya Ukimwi ni ‘dalili’ ya Upungufu wa Kinga Mwilini na siyo ugonjwa kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Aidha, tulisema kuwa, kwa tafsiri hiyo ya Ukimwi, ina maana kwamba kila mwenye Ukimwi siyo lazima ana Virusi vinavyosababisha Upungufu wa Kinga Mwilini na kila mwenye virusi (HIV Positive) siyo lazima ana Ukimwi. Hii ni dhana pana ambayo ikieleweka vizuri, umuhimu wa lishe mwilini nao utaeleweka vyema.
Katika mfululizo wa makala haya yanayoanza leo, tutaangalia ni kwa nini lishe ndiyo kila kitu kwa mtu anayeishi na virusi vinavyosababisha Ukimwi. Nimepata maombi mengi kutoka kwa wasomaji wetu wakitaka pia tuwakumbuke wenzetu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kwa kuwakumbusha lishe sahihi itakayowasaidia kuwapa kinga imara dhidi ya maradhi nyemelezi.
Kwa nini lishe bora ni muhimu zaidi kwa wenye virusi?
Lishe bora ni muhimu kwa wenye virusi vya Ukimwi kwa sababu hufanya mfumo wa kinga mwilini kuwa imara, hivyo kuusaidia mwili kupambana na maradhi ipasavyo. Pia lishe bora huboresha maisha. Lishe bora ni haki na wajibu wa kila mtu, hata kwa wale ambao hawajaathirika.
Bila lishe bora, matatizo ya kupungua uzito, kwashakoo, yataendelea kuwa mambo ya kawaida, licha ya kutumia dawa za kuongeza kinga na hali hiyo inaweza kuchangia kupatwa na magonjwa mengine hatari. Halikadhalika, lishe bora hufanya dawa unazokula zifanye kazi sawaswa.
Aidha, lishe bora pamoja na mazoezi, huweza kuondoa dalili za magonjwa kama vile kuharisha, kusikia kichefuchefu, kutapika, kusikia uchovu na shinikizo la damu na kisukari.
Hivyo basi, ili mtu mwenye virusi na Ukimwi aweze kuendelea kuishi maisha ya afya, ni lazima azingatie lishe hiyo bora. Pengine mtu utajiuliza, lishe bora ni ipi na unawezaje kuijenga? Hapa tunakuelimisha ifutavyo:
LISHE BORA NI IPI?
Lishe bora ni ile inayotokana na vyakula vya mbogamboga, matunda, nafaka halisi na vyakula jamii ya maharage, pamoja na vyakula vya protini vyenye mafuta kidogo. Vyakula tajwa hapo juu vina kiwango kikubwa cha virutubisho na vina mchango mkubwa sana kwenye ustawi wa afya yako kuliko vyakula vitokanavyo na sukari na mafuta pekee.
DONDOO ZA LISHE BORA
Kila siku hakikisha unakula mbogamboga na matunda ya kutosha, kwa nyakati tofauti, kiasi cha milo mitano hadi sita, sawa na vikombe vitatu. Kula mboga na matunda mchanganyiko ya rangi tofauti.
Kwa kuwa vyakula vya wanga (carbohydrates) ndivyo vinahimizwa kuliwa kwa wingi kwa mtu mwenye virusi, vyakula utakavyokula kwa siku, asilimia 50 vitokane na nafaka halisi (ugali wa mahindi yasiyokobolewa, mtama, ngano, uji wa ulezi, n.k).
Kula vyakula vya kuongeza protini mwilini ambavyo havina mafuta mengi, kama vile nyama ya kuku (bila ngozi), samaki, nyama steki isiyo na chembe ya mafuta (lean-meat) na bidhaa zitokanazo na maziwa yasiyokuwa na mafuta (low fat au fat free milk).
Punguza ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, vyakula vitamuvitamu na vinywaji baridi, kama vile soda, kwani vina virutubisho vya kutosha na huchangia kuamsha kiwango cha sukari mwilini.
Kila siku kula vyakula vingi vitokanavyo na mbegumbegu, kama vile karanga, korosho na vyakula jamii ya maharage, kunde, njegere, n.k.
Pia, katika ratiba yako ya kila siku, hakikisha unakunywa maji yasiyopungua lita moja (kwa uchache kama huna kazi nzito) au zaidi kulingana na shuguli unazozifanya. Maji ndiyo kila kitu katika uhai wako, ukiweza kuzingatia hayo, kamwe huwezi kusumbuliwa na maradhi mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment

New