My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, October 18, 2011

Mambo muhimu ya kufanya ili kijana ajikomboe kimaisha

Mada hii inaweza isiwahusu vijana peke yao lakini kwa kutambua wingi wa rika lao nimeamua kuwalenga wao ili kuwapa mbinu za kuweza kuwasaidia kujikomboa kimaisha. Hapa chini kuna muongozo wa kumfanya kijana afanikiwe kimaisha.

UNACHOAMINI
Njia ya kwanza ya kijana kujikomboa inaanzia kwenye kile anachoamini katika maisha yake. Katika hali ya kawaida mwanzo wa imani ya mwanadamu hutoka kwa wazazi wake na wakati mwingine mazingira atakayokulia.

Kwa mfano, wengi tumekuwa na dini kwa sababu tulizaliwa na wenye dini, kwa maana hiyo hata tunachokiamini hatukuchagua kwa akili zetu wenyewe. Kwa msingi huo, kama kuna walio na dini mbaya (nataja tu), wengi wao wameponzwa na kile walichorithishwa na wazazi wao.

Hali iko hivyo kwenye njia hii ya kwanza ya kijana kuelekea kwenye mafanikio. Wengi tumezaliwa na kurithishwa imani ya kutofanikiwa. Wazazi wetu walitulea kwa kutuambia maisha ni magumu, hatuwezi kufanikiwa, sisi ni masikini, duni na maneno kama hayo ya kukatisha tamaa.

Hata hivyo, walifika mbali zaidi ya hapo kwa kutuita majina “mbwa, nyani, wajinga, wapumbavu, vichaa na waliolaaniwa. Ushahidi wa hili upo mpaka leo, kuna wazazi wanawaita watoto wao majina ya aina hiyo.

Kwa hiyo, tukakua tukiamini kuwa sisi ni watu duni ambao hatuwezi kufanikiwa na kama tukiona mafanikio sehemu yoyote tunakuwa na mawazo kuwa, hiyo ni zawadi ya akina fulani wa ukoo mwingine, lakini siyo sisi.

Mawazo ya vijana wengi leo yanaamini kuwa, umasikini ni mzigo mkubwa usiokuwa na ufumbuzi. Kitaalamu mtu anapokuwa na mawazo ya kutokufanikiwa hawezi kufanikiwa kwa sababu mafanikio huhitaji nguvu na nguvu za mwili haziwezi kujitokeza kama hazikuvutwa kufanya kazi.

Kwa msingi huo, ili mtu aweze kufanikiwa lazima mawazo yake yakubali kuwa mafanikio ni sehemu ya lazima katika maisha. Jambo hili haliwezi kutokea mpaka kijana mwenyewe aliyelelewa kwenye mawazo ya kushindwa apigane vita na mawazo ya kutofanikiwa na kuyashinda.

Njia pekee ya kujikomboa na mawazo mgando ni kufuta na kupuuza kauli zote alizoambiwa na wazazi wake kuhusu maisha magumu na kuanza kuamini kuwa, maendeleo ni yake na kwamba muda unahitajika kuyafikia.

Wakati naanza safari ya kujikomboa kimaisha kutoka katika familia duni nilikabiliana na hali ya kuvunjwa moyo na watu wangu wa karibu wakiwemo ndugu zangu. Nakumbuka wakati nikiwa naishi na ndugu yangu mmoja wa ukoo aliniambia maneno haya: “Wewe utakuwa mtu usiyekuwa na mwelekeo na kamwe huwezi kufanikiwa.”

Nikiwa katika hali hiyo ya utumwa wa mawazo siku moja ndugu yangu aliniambia kuwa hataki kuishi na mimi na kwamba ilinipasa kuondoka nyumbani kwake. Nakumbuka nililia sana siku hiyo.

Wakati nikiwa kwenye maisha magumu kiasi hicho nilikutana na rafiki yangu mmoja aliniambia maneno haya: “RICH IPO SIKU UTAFANIKIWA KWA KUWA UNA AKILI NYINGI NA UWEZO WAKO NI MKUBWA.”

Usiku sikulala nilikuwa natafakari juu ya akili zangu na uwezo wangu wa kufanikiwa, naweza kusema maneno hayo yalikuwa ni mwanga mpya katika maisha yangu na mwanzo wa kufanikiwa kwangu.

Nakushauri kijana mwenzangu kuanzia leo uyakatae mawazo ya kushindwa na kukubali udhaifu wako kwamba huwezi kufanikiwa kwa sababu yoyote ile, sema LAZIMA UFANIKIWE KWA KUWA UWEZO HUO UNAO.

No comments:

Post a Comment

New