My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, October 18, 2011

Yaliyofanyika sasa katika nchi yetu yanatufanya tumkumbuke Mwalimu Nyerere

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

MUNGU ni muweza wa yote anachoamua hakuna wa kutengua, sote tumshukuru kwa wema wake unaotuwezesha tuvute pumzi ambayo inatufanya tuweze kuwajibika.

Baada ya kusema hayo niweke wazi kwamba kuna mambo yanayofanyika siku hizi ukiyatafakari utakumkubuka Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hivi sasa ni jambo la kustaajabisha kuona baadhi ya viongozi wetu wakipalilia udini, ambao unaingizwa katika siasa. Sitapenda kutoa mifano mingi ya nyuma kwa mfano, tukio la Mkuu wa Wilaya ya Igunga kutolewa mkutanoni na vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kisha kitambaa chake cha kichwani au ushungi kuvuka, baadhi ya viongozi wasiojali hatari ya tukio hilo wakaliingiza katika udini.

Viongozi hao walidai kwamba alivuliwa hijabu, walikuwa wakiangalia upande mmoja tu kuwa watavuna kura za upande fulani huku wakisahau kuwa wanasababisha ufa mbaya sana wa kitaifa. Hivi hawakujiuliza kuchochea udini kwa nia ya kupata kura ni hatari?

Mwalimu Nyerere tunamkumbuka kwa sababu alikataa udini katika nchi yetu na ndiyo maana kifo chake kilichotokea miaka 12 iliyopita yaani mwaka 1999 kinafanya Watanzania wahuzunike hadi leo.
Hii ni kutokana na upendo na uaminifu wake kwa taifa lake na watu wake uliomfanya awe lulu na kipenzi cha wananchi wa dini zote.

Nyerere alikuwa kiongozi mwenye maadili mema ambayo kila mwananchi alitaka kuyaiga. Alikuwa na dira na mwelekeo uliotoa matamanio ya kulipeleka taifa kwenye mafanikio katika mazingira ya amani, umoja na mshikamano.

Mwalimu Nyerere tunamkumbuka kwa kuwa alikuwa kiongozi mwenye maono ambaye alihubiri umoja na upendo na alisifika duniani kote kwa falsafa yake kwamba binadamu wote siyo tu wako sawa lakini pia ni ndugu na aliamini kuwa Afrika ni moja na akajiingiza katika kupigania uhuru wa nchi zingine za bara hili.

Ndiyo maana Tanzania, pamoja na uchumi wake duni, iligeuka kuwa kimbilio na hifadhi ya wakimbizi kutoka kila pembe ya dunia. Upo ushahidi kuwa hakuwa mbaguzi kwa misingi ya dini, jinsia, kabila au rangi. Kwa kufanya hivyo, Tanzania ilijipambanua na viongozi wake kuwa vifua mbele kwenye jumuiya ya kimataifa kwamba nchi yao ni kisima cha amani wakati ambapo nchi nyingi barani Afrika zilikuwa zimegubikwa na migogoro, mifarakano na vita ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na mifumo ya kifisadi na siasa za ghiliba.

Siasa za udanganyifu hivi sasa zinaota mizizi katika nchi yetu. Mfumo wa maisha unabadilika na baadhi ya viongozi siyo viongozi wa wananchi tena bali wanafanya kazi kwa faida ya familia zao,kitu ambacho ni hatari, si kwa umoja wa kitaifa bali pia kwa familia zinazofanya hivyo kwa sababu wananchi wa leo wanaona wanavyopora mali za umma. Enzi ya Mwalimu kulikuwa hakuna mafisadi, leo eti kiongozi aliyekuwa anaaminiwa na taifa anatuhumiwa kufuja mabilioni ya shilingi.

Ndugu zangu, tunashuhudia serikali ikishindwa kununua magari kwa ajili ya wagonjwa na badala yake inanunua vibajaji kutokana na kile kinachosemwa kuwa ni ufinyu wa bajeti, lakini ndani ya wizara hiyo, kiongozi anajenga mahekalu na kujinunulia ‘mashangingi’, watu wanaona.

Tunamkumbuka Mwalimu kwa sababu ukienda kwenye zahanati au kituo cha afya daktari atakuandikia dawa za kununua lakini viongozi wao wakiumwa wanaruka na ndege na kwenda kutibiwa nchini India, watu wanaona.

Tunamlilia Nyerere maana alianzisha mashirika ya umma zaidi ya 400, yakauzwa, wakapewa wawekezaji, wakawa wanaendesha kwa faida. Kwa nini sisi tufeli? Hatuna wasomi? Faida wanayopata wageni hao wanapeleka kujenga kwao huku sisi tukilia njaa.

Aidha, Nyerere angekuwa hai asingekubali ujinga wa sakata la Richmond, eti mtambo wa kufua umeme unaletwa, wanasiasa wanaukataa lakini baadaye wajanja wanawauzia watu wengine halafu, Tanesco wanauziwa umeme. Baadaye tunaambiwa viongozi wetu wasomi wamevunja mkataba na Dowans, wanapongezana.

Baada ya siku chache Tanesco inashitakiwa na kushindwa kesi, inaamriwa kulipa shilingi bilioni 94. Wasomi wetu wanapinga Mahakama Kuu ya Tanzania, baada ya siku chache tunaambiwa tumeshindwa kesi na sasa tunatakiwa kulipa shilingi bilioni 111 kutokana na riba.

Ndugu zangu, nasema hayo kwa uchache inafanya tumkumbuke Nyerere huku tukimwaga machozi, hakika aliona hatari ya kuweka rehani utaifa na uhuru wetu.

Haiba na uaminifu wake vilimpa karaha ya kuheshimiwa hata na mahasimu wake wa ndani na nje kutokana na kusimamia ukweli na kupigania haki za wanyonge kote duniani.

Huyo ndiye Mwalimu Nyerere ambaye leo Watanzania tunamlilia, mtu aliyeogopa kujijengea hekalu la kuishi na hata pale alipoombwa kujengewa akasema, “Mimi siyo tembo.”

Wakati tukiadhimisha kumbukumbu ya kifo chake na miaka 50 ya kuzaliwa kwa taifa letu, ni vyema basi tukazingatia kwa dhati na kutekeleza kwa vitendo maelekezo na mafundisho yote aliyotuasa, na hasa viongozi wetu.

Ni bahati mbaya kwamba dalili zote zinaonyesha kuwa, Watanzania hasa baadhi ya viongozi tunaowapa dhamana ya kutuongoza siyo tu wanaanza kumsahau Mwalimu Nyerere, bali pia wametupilia mbali maadili ya taifa na mambo yote aliyoyasimamia na badala yake wanajipendelea wao kula keki ya taifa.

Chanzo cha tatizo hilo ni viongozi wetu ambao wamelipiga teke Azimio la Arusha lililoweka misingi ya umoja na usawa na kuifanya Tanzania kiwe kisiwa cha amani na mshikamano. Watu wanasaka uongozi katika nchi hii ili kupata utajiri, siyo tena kwa lengo la kuwatumikia wananchi hasa wa ngazi ya chini.

Mustakabali wa taifa letu uko hatarini iwapo viongozi wetu hawatarudia misingi ya Azimio la Arusha na kumuenzi Mwalimu kwa vitendo badala ya usanii tunaouona sasa kwa viongozi. Viongozi wanahonga au kutoa rushwa ili wapate uongozi ili wafanye nini? Mwalimu aliwahi kuhoji, kiongozi kama huyo atarudishaje gharama hizo? Ni wazi kuwa atakula rushwa.

Ndiyo maana sasa mfumuko wa bei haudhibitiwi, sukari inavushwa nje, bei ya vyakula inakuwa juu, nauli zinapanda kiholela tofauti na enzi za Nyerere ambaye alisimamia rasilimali za nchi na alihakikisha zinawanufaisha wananchi wote. Rasilimali hizo sasa zinakwapuliwa na watu wachache, lakini wanaofanya hivyo watambue kuwa siku moja wataondolewa madarakani na wapiga kura wao

No comments:

Post a Comment

New