My Web

Emmanuel

CONTACT

Thursday, October 27, 2011

Utandawazi katika vyakula ndio unaotumaliza - 2

WIKI iliyopita tuliangalia jinsi ambavyo utandawazi ulivyoathiri vyakula tunavyokula kila siku hivyo kujikuta tunakabiliwa na maradhi sugu bila kujua chanzo ni chakula tunachokula, wiki hii tunaendelea na sehemu ya mwisho ya makala haya.

Vyakula na mbogamboga navyo haviko salama. Hivi sasa kuna vita kali inaendelea ya kupinga uoteshaji wa mazao ya chakula kwa njia ya kisayansi inayojulikana kama GMO (Genetically Modified Organisms). Njia hii huongeza idadi ya mavuno na ukubwa wa matunda kuliko kawaida. Mahali ambapo ulikuwa ukivuna magunia mawili ya nafaka, unaweza kuvuna magunia 50. Matunda yanayolimwa kwa mtindo huu, nayo huwa makubwa kuliko kawaida.

Pamoja na wingi wa mazao na ukubwa wa matunda yanayopatikana kwa utaalamu huo, lakini imegundulika mazao hayo kuwa na athari mbaya kwa mlaji.

Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Seeds Of deception’ cha mwandishi mwanaharakati wa mambo ya lishe, Jeffery Smith, ulaji wa vyakula hivi una uhusiano mkubwa na ukosefu wa uzazi, vifo vya watoto wadogo, upungufu wa kinga mwilini, kuzeeka, vifo vya ghafla na kujaa kwa sumu mwilini.

Hii inatokana na ukweli kwamba utayarishaji wa mbegu hizo na uoteshaji wa mimea yake hadi ukuzaji wa mazao yake, hufanyika kwa njia za kisasa badala ya njia ya asili na hivyo kuotesha mazao yasiyokuwa na faida mwilini.

KUKU NA MAYAI
Kuku na mayai navyo ni vyakula vinavyoliwa kwa wingi hivi sasa mijini. Walaji wengi wa kuku na mayai hula mayai na kuku wa ‘kizungu’. Hapa napo pana tatizo kubwa la kiafya kwa sababu vyakula wanavyolishwa kuku hao havikubaliki kiasili na kiafya.

Kwa maana hiyo, mayai yatokanayo na kuku wa kizungu waliolishwa vyakula visivyo vya asili na kulishwa madawa mbalimbali, nayo siyo salama kiafya. Faida iliyokusudiwa kupatikana kwenye mayai inakosekana na mayai kugeuka kuwa hatari kiafya.

Ukiacha mayai, hata nyama yake nayo inakuwa siyo salama tena kiafya kama ile ya kuku aliyefugwa kienyeji. Tumesikia hadithi nyingi za watu kupatwa na matatizo mengi ya kiafya kutokana na kupenda kula mayai na nyama za kuku wa kizungu.

UNGA WA MAHINDI
Ugali ukiwa ndiyo chakula kikuu na kinacholiwa na idadi ya watu wengi nchini, kimekuwa ndiyo chanzo cha magonjwa hatari kutokana na aina ya unga unaotumika kupikia ugali huo.

Unga unaozalishwa kwa wingi viwandani na kusambazwa nchi nzima, ni sembe nyeupe ambayo kwa kawaida huwa imeondolewa virutubisho vyake vyote muhimu na kubaki makapi ambayo hayana faida mwilini, zaidi huwa chanzo cha magonjwa hatari kama kisukari, shinikizo la damu na mengine.

Mfumo mzima wa maisha umeharibika na ndiyo maana maradhi nayo yameongezeka na yataendelea kuongezeka mpaka pale mfumo mzima wa uandaaji, usambazaji na ulaji wa vyakula utakapobadilika. Kutokana na mazingira yaliyopo, karibu kila chakula tunachokula ‘kimechakachuliwa’, tunalazimishwa kula hivyo hivyo, ama kwa kutokujua au kwa kukosa hiyari (alternative).

Naomba tuamke kwa kupenda sana kusikiliza na kusoma maandiko mbalimbali yanayohusu lishe na ulaji sahihi wa vyakula na umuhimu wake katika mwili na maisha ya binadamu na Mungu atakupa afya njema.

No comments:

Post a Comment

New