My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, July 30, 2012

MAANDALIZI YA WIZARA KUSHIRIKI KATIKA MAONYESHO YA NANENANE DODOMA YAMEKAMILIKA


Wizara ya Maliasili na Utalii itashiriki katika maeonyesho ya Nanenane ambayo yatafanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma tangu tarehe 1 Agosti 2012. Kama kawaida Wizara imeandaa banda moja kubwa ambalo italitumia pamoja na Mashirika, Wakala, Taasisi zake na wadau wa Wanyamapori, Misitu, Nyuki Malikale na Utalii.
Maandalizi ya banda la Wizara ya Maasili na Utalii ambalo lina sehemu kuu tano yamekamilika. Sehemu hizo tano ni:
(i) banda kuu ambapo maelezo yatatolewa na machapisho kugawiwa kwa wageni,
(ii) Bustani ya miti;
(iii) Shamba la Nyuki;
(iv) Wanyamapori hai;
(v) Mashindano ya ufugaji Bora wa nyuki bora.
Katika sehemu ya Wanyamapori hai kutakuwa na aina 20 za wanyama. Leo jioni tarehe 29/7/2012 Wanyama watakaowekwa kwenye mabanda maalum yaliyoandaliwa tayari kwa maonyesho ni Simba, Chui, Tumbili, Kobe, Kanu, Fisi madoa, Fisi Mraba, Sokwe Mtu na Chatu. Wanyama wengine na ndege watawasili leo usiku tayari kuwekwa kwenye mabanda yao kesho.
Aidha katika banda la Maliasili kutakuwa na maonyesho ya asali kitaifa ambayo yameandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwa njia ya ushindani. Katika mashindano hayo wafugaji wa nyuki walitembelewa na wataalam katika sehemu wanakofugia na kushindanishwa kwa kuzingatia ufanisi katika ufugaji na utunzaji bora wa mazao ya nyuki hususan asali. Washindi watapewa zawadi na Mgeni Rasmi siku ya kilele cha maonyesho haya ya Nanenane tarehe 8/8/2012.
Kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu ni: “Kilimo Kwanza: Zalisha kisayansi na kitekenolojia kukidhi mahitaji ya ongezeko la mahitaji ya watu”.
Kutokana na kauli mbiu hiyo Wizara itawelimisha wananchi kuhusu uhusiano wa shughuli za Maliasili na Utalii na “Kilimo Kwanza”. Kwa mfano wananchi wataombwa kuhifadhi misitu na kupanda miti kwa kuwa misitu inachangia katika kuleta mvua inayofanikisha kilimo. Vilevile vyanzo vya mito inayofanikisha kilimo cha umwagiliaji ni katika misitu.
Aidha wanyamapori hufanikisha utalii ambao huchangia asilimia 26 ya pato la fedha za kigeni nchini. Fedha hizo za kigeni zinatumika katika kununulia zana za kilimo, kama vile matrekta. Pia biashara ya mazao ya Maliasili huleta maduhuli ambayo yanapelekwa Hazina na hatimaye kutumika katika kufanikisha kilimo, kama vile kununua pembejeo.
Wananchi wanaoishi katika mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani wanakaribishwa kutembelea banda la Maliasili katika maonyesho ya Nanenane Dodoma ili wapate utaalam wa kushiriki katika shughuli za kuhifadhi na kuendeleza Maliasili kwa manufa yao.
[MWISHO]George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 29 Julai 2012

No comments:

Post a Comment

New