My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, July 2, 2012

Madiwani wamkataa DC Shinyanga

Suzy Butondo Shinyanga.
MADIWANI wa Manispaa ya Shinyanga wamemkataa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga AnnaRose  Nyambi   kutokana na kitendo chake cha kushinikiza wakulima wa kijiji cha Mwamashele katika Manispaa  hiyo wanyang’anywe  mashamba yao  na Kambi ya Jeshi la Wananchi  wa Tanzania (JWTZ)  kikosi cha 516KJ Kizumbi  yaliyopo kijijini hapo.

 Madiwani hao walichukua huo  uamuzi  katika kikao cha baraza la madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Shinyanga.

Madiwani hao walidai kukerwa na kitendo hicho na pia kukasirishwa na  baadhi ya Askari wa Jeshi  hilo ambao walikwenda kijijini hapo  wakiwa na bunduki na  kuwalazimisha wamiliki wa  mashamba hayo  kuruka kichura bila kosa lolote.

“Nasema  sina imani na Mkuu wa Wilaya, huyu anafaa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kambi ya Jeshi ya Kizumbi na siyo Mkuu  wa Wilaya ya Shinyanga yetu hii, hatufai kabisa kwa sababu hakuna anachotusaidia, badala ya kusaidia wananchi anawakandamiza ”  alisema Sebastian  Peter  diwani wa kata ya Ngokolo.

Madiwani hao walidai kushangazwa na uamuzi wa Mkuu wa Wilaya hiyo kukubaliana na uongozi wa  kikosi cha 516KJ  kupora  eneo  lenye ukubwa wa hekta  za mraba 850 mali ya wananchi wa kijiji  cha Mwamashele ambalo linajengwa mradi wa  kilimo cha umwagiliaji  wenye thamani ya shilingi Milioni 275.

Aidha walisema  kikosi cha 516KJ  Kizumbi kiliomba kupewa eneo lililoko katika Vijiji vya Mwamashele na Nhelegani  kwa kufuata taratibu zote mwaka 1979 ambapo  wananchi walikubali   kutoa eneo hilo na lilipimwa na  wataalamu wa Ardhi na kuliwekea  mawe ya  mipaka kati ya  (JWTZ)  na  wananchi  wa vijiji hivyo.   

Walisema walishangazwa na kitendo cha askari hao  mwaka usiofahamika walikwenda kung’oa mawe yaliyowekwa na wataalamu wa ardhi  kutenganisha eneo la  kambi ya Jeshi na vijiji na kujiongezea eneo  bila ya kuwashirikisha wakazi wa Mwamashele, wataalamu wa Ardhi,  au   viongozi  wa Halmashauri ya  Manispaa ya Shinyanga.

Walieleza pamoja na  askari wa (JWTZ) kujiongezea eneo kiholela bila ya kufuata utaratibu pia walimpa kazi ya kuchora ramani ya eneo hilo  askari  wa Jeshi hilo aliyetambuliwa kwa jina la Ignus  Valalia na kupitishwa na Wizara ya Ardhi  Juni 13, mwaka 2005 huku wananchi wa kijiji cha Mwamashele wakiwa hawajui  kuwa eneo lao lilikwisha porwa na  askari wa kikosi cha 516KJ cha Kizumbi.    

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamashele  Daniel  Sweya alikiri kuporwa  kwa mashamba yao bila ya wao kujua na kuongeza kuwa eneo ambalo  walilitoa kwa askari wa jeshi hilo walioko katika kikosi cha 516KJ wanalifahamu na hawana madai nalo kwa sababu hata wananchi waliokuwa ndani ya eneo hilo walikwisha lipwa fidia na Jeshi.

“Sisi tulishalipwa  fidia ya maeneo yetu  kisha tukahamia katika maeneo   yaliyobakia, lakini tumesikitishwa sana na kitendo cha Askari wa Jeshi la Wananchi leo kuanza kudai kuwa hili ni eneo lao wakati miaka mingi tuko hapa na tumeshajenga  nyumba zetu na tunaishi , inamaana waliomba kutoka kwa nani eneo hili au wanatuonea tu “   alisema Sweya. 

No comments:

Post a Comment

New