My Web

Emmanuel

CONTACT

Saturday, July 14, 2012

Vitambulisho vipya vya uraia vya Tanzania kuimarisha usalama na uchumi

 
Mpango wa kadi za vitambulisho vipya vya taifa umeanza mwezi uliopita jijini Dar es Salaam katika jitihada za kuimarisha usalama na kuongeza mapato ya serikali, kwa mujibu wa Naibu Kamishna Mkuu wa Polisi, Issaya Mangulu. Mpango huo unawataka raia wa Tanzania na wa kigeni wanaokaa nchini humo kwa angalau miezi sita kujisajili na walio na umri wa kuanzia miaka 18 kujisajili na kutembea na kitambulisho. 

"Kimsingi, vitambulisho hivi vitasaidia mfumo wetu wa kuwafuatilia wahalifu," Mungulu aliiambia Sabahi. "Taarifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) zitatumika (wakati wa uchunguzi) kujua historia ya mshukiwa, ambayo inajumuisha anapoishi au kufanya kazi na mengine kama hayo."

Alama za vidole na picha za wenye vitambulisho hivyo zitachukuliwa kurahisisha utaratibu wa kuwatambua watu hapo baadaye. Kuwatambua watu wanaoishi na kufanya kazi nchini Tanzania ni jambo la msingi katika kuhakikisha usalama, hasa kutokana na idadi isiyojulikana ya wakimbizi ambao wameingia kutoka nchi jirani zenye vita na migogoro, alisema. Kwa zaidi ya miaka 40, Tanzania imepokea wakimbizi kutoka Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na baadhi ya wahalifu wanaweza kuja kupitia njia hiyo hiyo, alisema Mungulu.

Kutokana na wimbi hilo la wakimbizi wanaoingia nchini, kuwa na mfumo wa kutambua utaifa wa mtu, hadhi ya kisheria na taarifa nyingine kunakuwa muhimu kwa juhudi za jumla za usalama, alisema. Taarifa za vitambulisho vya taifa zitaunganishwa na mifumo mingine ya kitaifa, kama vile mfumo wa namba za posta, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania, taarifa za polis,i na mashirika ya usalama ya kimataifa kama vile Interpol. Mafungamano ya mashirika kadhaa, ya ndani na ya nje, yatasaidia kufikia lengo la muda mrefu la usalama na uchumi, alisema Mungulu.

Hadi sasa, waajiriwa wa serikali na wataalamu wanaofanya kazi kwenye mabenki wamepewa kipaumbele na kusajiliwa, alisema Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu, katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Mpango huo ulioanza Septemba, utasambaa sehemu zote za nchi. Usajili unatarajiwa kukamilika mwaka 2014, lakini utaendelea hata baada ya hapo kuwasajili raia ambao wanafikia umri wa kulazimika kuwa na kitambulisho. "Usajili utakuwa utaratibu wa kuendelea," alisema Maimu.

Kwa ajili ya kujiandaa vyema na hatua hii, Maimu alisema NIDA ilifanya programu ya majaribio mwanzoni mwa mwezi Juni katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. Zoezi hilo liliisaidia mamlaka hiyo kuyagundua na kuyapatia ufumbuzi mapungufu yaliyoonekana kwenye mchakato huo, alisema. "Kama unavyojua, Dar es Salaam ndio mji mkubwa kabisa nchini. Tukifanikiwa kutoa vitambulisho Dar es Salaam, mradi huu utafanikiwa nchi nzima," Maimu aliwaambia waandishi wa habari. Vitambulisho vitatolewa bure kwa Watanzania wote, ambapo Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) litalipia gharama za vitambulisho vya wakimbizi.


Vitambulisho vinaunganishwa na huduma za kijamii, mikopo ya benki

Chini ya mpango huo mpya, itakuwa ni lazima kwa raia wa Tanzania kujisajili na kutembea na kitambulisho cha uraia. Kuvunja sheria hiyo kunaweza kupelekea kifungo cha hadi miezi sita, alisema Meneja Mahusiano wa NIDA, Thomas William. "Baada ya yote, kitambulisho hicho kitakuwa kinaunganishwa na mifumo ya huduma za kijamii. Ukikataa kujisajili au kutoa taarifa za uongo, hilo litakuwa na athari kwako mwenyewe. Utakuwa hustahiki kupata huduma nyingine za kijamii hadi utakapokuwa na kitambulisho hicho. Kwa hivyo, watu lazima wawe navyo," William aliiambia Sabahi.

Vitambulisho hivyo vitatolewa na kampuni ya Malaysia iitwayo Iris Corporation Berhad, ambayo imeshinda zabuni ya kutoa vitambulisho milioni 25. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 200 (dola milioni 124) na unafadhiliwa na serikali ya Tanzania. Joseph Bwakyayo, 55, mfanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara jijini Dar es Salaam, aliiambia Sabahi kwamba kuwatambua wakopaji kutawasaidia wakopeshaji kutathmini hatari na gharama za mtu binafsi na kuamua juu ya uwezo wa kukopesheka wa kila mkopaji, ambako kutaifanya mikopo iwe rahisi zaidi kufikiwa na raia. "Watanzania hawakusajiliwa na ni gharama kubwa kuwatambua waombaji wote wa mikopo kuhakikisha kuwa benki zinawakopesha watu wanaostahiki. Ni kama kucheza kamari," alisema Bwakyayo.

Bwakyayo alisema mara kwa mara wakopeshaji hulazimika kuthibitisha mambo mepesi kama eneo la makaazi kwa kutembelea nyumbani au kwenye biashara ya mkopeshwaji, na ambako pia huweza kukutana na utapeli wa wale wanaojifanya kuwa ni wamiliki wa biashara fulani. "Kufidia hatari kama hizo, tunaweka kiwango kikubwa cha riba," alisema. Pamoja na kuziweka gharama za kuthibitisha juu ya wakopaji, baadhi benki hulipisha hadi asilimia 40 kuepuka hatari ya kufilisika, alisema.

No comments:

Post a Comment

New