My Web

Emmanuel

CONTACT

Monday, July 2, 2012

Mbowe kupangua Baraza Kivuli la Mawaziri


Mussa Juma, Dodoma
KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe leo anatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika safu ya baraza kivuli la mawaziri.Habari za uhakika kutoka katika kikao cha ndani cha wabunge wa Chadema ambacho kilifanyika jana, zimebainisha kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuboresha utendaji wa mawaziri kivuli katika nafasi zao.

Mbowe alithibitisha baadaye kuwapo kwa mpango huo, kuwa mabadiliko hayo pia yanalenga kujaza nafasi za wabunge wa Chadema ambao hawapo kwa sasa, akiwamo Godbless Lema aliyekuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani.

Nafasi zingine zinazotarajiwa kujazwa ni ile iliyoachwa na Marehemu Regia Mtema aliyekuwa Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira na nafasi ya Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini ambaye hatarajii kurejea karibu bungeni kutokana kukabiliwa na majeraha baada ya kupata ajali.

“Wewe nani amekupa hizi taarifa, ila nakuthibitishia ni kweli leo nilikuwa na kikao na wabunge, na ni kweli tutafanya mabadiliko makubwa ya mawaziri kivuli,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe alikataa kusema kama katika baraza hilo, atawaingiza wabunge wa vyama vingine vya upinzani ambao wamekuwa wakiomba kushirikishwa kwa muda mrefu.

Mbali na Chadema ambayo kwa sasa inmaunda kambi hiyo peke yake, bungeni vipo vyama vingine vitatu vya upinzani ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP.

Ingawa Mbowe hakutaka kueleza kwa undani, habari za uhakika zimeeleza kuwa miongoni mwa mawaziri kivuli wanaotarajiwa kubadilishwa ni Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu.

“Tutakuwa na mabadiliko ya nafasi mbali mbali na pia tutajaza nafasi zilizo wazi, pia naomba ieleweke lengo ni kuboresha tu utendaji wetu wa baraza kivuli,” alisema Mbowe.Katika mabadiliko hayo, upo uwezekano wa Mbowe kuingiza katika baraza hilo baadhi wabunge wa upinzani, baada ya kutazama mienendo na ushirikiano naiba yao, kama alivyoeleza wakati anatangaza baraza hilo mwaka 2011.
Ajibu tuhuma za wabunge

Akizungumzia tuhuma zilizotolewa na wabunge wa CCM, Mwigulu Nchemba  (Iramba Magharibi) na Mbunge Livingstone Lusinde (Mtera), kuwa anawahadaa Watanzania kwa kukataa gari kuu kuu la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), lakini akageuka kwa mlango wa nyuma na kuchukua jipya, Mbowe alisema kauli hizo ni za kisiasa.

Mbowe alisema ni kweli kuwa hivi sasa analitumia gari la KUB ambalo alilikataa kwa kipindi cha miezi sita bila kulitumia, lakini Serikali imekataa kubadili sera yake za kuacha kununua magari ya kifahari.

“Mimi nilikataa kwa miezi sita, nilikuwa silipwi gharama zozote za mafuta ikiwamo  hata hii ya kila siku ya wabunge na gharama ya mafuta ya kutoka jimboni na kwenda jimboni, na nia yangu ilikuwa ni kuionyesha Serikali kuwa tunaweza kukataa haya matumuzi mabaya lakini, wamegoma,” alisema Mbowe.

Alisema kimsingi, asingeweza kugoma milele kwani lengo lake lilikuwa ni kutoa msukumo ambao ungewezesha magari yote ya kifahari yapigwe mnada.

“Hawa jamaa hawataki kubadilika, nimeona suluhu hapa sio tu kukataa gari lao bali ni kuungana na wadau wengine kuwang’oa madarakani kwa sababu hata katika bunge la mwaka huu, hawajasema kama kuna sera rasmi ya kupunguza matumizi kwa kununua magari ya kifahari,” alisema Mbowe.

Kuhusu kugomea posho ya Sh80,000 ya bunge na kuchukua posho ya Sh 2 milioni kwa mwezi kama KUB, alisema suala hilo anayepaswa kuulizwa ni Katibu wa Bunge, lakini mtu anapokuwa kiongozi wa upinzani bungeni ana stahili zake ambazo zimepangwa.

“Unapokuwa kiongozi wa upinzani kuna stahili nyingi wanapanga sasa zipo kisheria hata kama ukikaa hapa kuna mambo ya kisheria na kiutaratibu, lakini kama nilivyosema awali kikubwa hapa ni kuiondoa Serikali tu, ili kufuta mambo haya,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo, pia alikanusha tuhuma zilizotolewa na Nchemba kuwa anasomesha mtoto wake chekechea katika shule ya kimataifa kwa dola 15,000 (karibu Sh20 milioni) kwa maelezo kuwa hana mtoto anayesoma chekechea, watoto wake wote ni wakubwa.

No comments:

Post a Comment

New