My Web

Emmanuel

CONTACT

Friday, July 20, 2012

Tume ya Katiba yasitisha kukusanya maoni

     

Mwandishi Wetu
TUME ya Mabadiliko ya Katiba, imesitisha Mikutano ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Mkoa wa Kusini Pemba kutokana na ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea juzi.

Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Tume hiyo ya Katiba, ilieleza kuwa mikutano iliyositishwa ni ile iliyopangwa kufanyika kuanzia jana hadi Jumamosi maeneo ya Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri, Pujini, Gombani na Wara, visiwani Zanzibar.

“Tume imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali ya Meli ya MV Skagit na imesitisha mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokuwa inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Tume ya Katiba  ilisema mchakato wa kukusanya maoni utaendelea Jumapili na kuwa ratiba ya mikutano katika maeneo yaliyositishwa itatolewa baadaye.

Hata hivyo, tume hiyo imeeleza kuwa mabadiliko hayo hayahusu mikutano ya kukusanya maoni inayoendelea kufanyika katika mikoa sita (6) ya Tanzania Bara, ambayo ni Pwani, Tanga, Dodoma, Shinyanga, Kagera na Manyara. 

“Tume inawaomba wananchi wa mikoa hii kuendelea kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

 “Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa pole kwa wafiwa, majeruhi na wote walioguswa na ajali hii na tunamwomba Mwenye Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na majeruhi wote wapone kwa haraka.”


Kukusanya maoni

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kuanzia Julai 2, mwaka huu.
Tayari tume hiyo imesambaza ratiba zake za ukusanyaji wa maoni katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.

Tume hiyo inaendesha kazi zake kupitia mikutano ya hadhara inayoitishwa maeneo mbalimbali ambapo wananchi na kupewa fursa ya kutoa  maoni yao kwa uwazi, uhuru na utulivu.Wananchi pia wamepewa fursa ya kutoa maoni yao kupitia mawasiliano ya mtandao wa kompyuta katika tovuti ya  www.katiba.go.tz na vile vile kwa njia ya posta.

No comments:

Post a Comment

New