My Web

Emmanuel

CONTACT

Friday, July 20, 2012

Operesheni kata umeme yakusanya Sh86 milioni

    
Ibrahim Yamola
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) Kanda za Ilala na Temeke, Dar es Salaam limeendelea na operesheni za kukata umeme kwa wateja wanaodaiwa kulihujumu.

Wakizungumza kwenye operesheni iliyofanyika jana kwa nyakati tofauti mameneja hao, walieleza jinsi operesheni inavyosaidia kukamata wahalifu wa mita za umeme na ufanisi uliopatikana tangu kuanza.
Meneja wa Kanda ya Ilala, Athanasius Nangalia alisema kuanza kwa operesheni hiyo mwezi mmoja uliopita, wamefanikiwa kukagua wateja 4,700 na kukamata wezi wa umeme 51 ambao kutokana na faini walizolipa wamekusanya Sh45 milioni.

Nangali alisema licha ya ukusanyaji huo, waligundua watu wanaojiunganishia umeme bila utaratibu kwa kujiwekea nguzo zao wenyewe, lakini wamedhibiti vitendo hivyo kwa kukamata nguzo 18 maeneo mbalimbali.

Katika zoezi hilo lililofanyika juzi eneo la Upanga liliambatana na vituko kutoka kwa wenye nyumba, baada ya kujifungia ndani na kukataa wakaguzi hao kuingia kwenye nyumba hizo.
Wakaguzi hao waliamua kubandika ujumbe kwenye mageti hayo unaoeleza namba za mwisho za mita zilizosomwa.

Kanda ya Temeke operesheni hiyo ilimefanyika eneo la Kigamboni na kufanikisha kutiwa mbaroni kwa watu watatu, ambao wanatuhumiwa kujihusisha na wizi wa umeme.
Mfanyabiashara mmoja alikutwa akiwa na mita mbili ambazo licha ya kutumia umeme, lakini hazisomi na wala umeme hauishi hatakama akiwasha vifaa vyake vyote, hali iliyowalazimu wakaguzi hao kukata umeme na kumshikilia kwa mahojiano zaidi.

Meneja kanda hiyo, Richard Mallamia alisema vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea lakini mwisho umefika, kwani kutokana na mifumo inayotumika kwa sasa wanamtambua moja kwa moja mwizi wa umeme bila kwenda nyumbani kwa mteja.

“Hili zoezi siyo gumu sana kwa sababu tunakwenda sehemu ambazo tuna hakika kuna watu wanaiba umeme, kweli tukifika tunawakamata,” alisema Mallamia.
Hadi sasa watu 13 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya kukamilika taratibu za mashtaka kutokana na wizi huo.

Alisema Sh40 milioni kimekusanywa kutokana na faini na kwamba, Sh89 milioni zinapotea kwa mwezi kutokana na wizi wa umeme.

No comments:

Post a Comment

New