My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, April 11, 2012

MAZISHI YA KANUMBA KAMA NYERERE

Na Waandishi Wetu
HUZUNI, simanzi na majonzi vimetawala katika mazishi ya marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ ambayo yamevunja rekodi hadi kufananishwa na yale ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 kufuatia umati uliohudhuria kumuaga.
Katika mazishi hayo, Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, jana Jumanne lilizizima kwa vilio pale maelfu ya wakazi wake walipokusanyika kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni kuuaga mwili wa staa huyo wa filamu aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake maeneo ya Vatican, Sinza.
Mwili wa marehemu Kanumba ulichukuliwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya misa na kuagwa kabla ya kupelekwa kupumzishwa katika nyumba ya milele kwenye makaburi ya Kinondoni.
Msafara uliokuwa na magari zaidi ya kumi huku ukilindwa na ‘difenda’ tatu za askari wakiwa na mbwa, farasi ulilazimsha baadhi ya barabara kufungwa kama ilivyokuwa kipindi cha kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

DK. BILAL MGENI RASMI
Baada ya kuwasili katika viwanja hivyo, mgeni rasmi makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, saa 4:00 asubuhi, ilifanyika misa iliyoongozwa na msaidizi wa Askofu wa Kanisa la African Inland la Chang’ombe, Dar.

MAELFU WASHINDWA KUMUAGA
Hali haikuwa shwari katika mazishi ya nguli huyo wa filamu nchini kufuatia maelfu ya watu waliohudhuria kushindwa kumuaga na kumzika mpendwa wao kutokana na wingi wa watu ambapo inakadiriwa zaidi ya watu 60,000 walihudhuria.

MASTAA WAISHIA KUPIGWA VIKUMBO
Utaratibu wa kuuaga mwili wa marehemu ulivurugika na watu wote kushindwa kupata nafasi kufuatia umati mkubwa, hivyo zoezi hilo lilifanikiwa kwa wanafamilia na waheshimiwa pekee huku mastaa wenzake wakiishia kupigwa vikumbo.
Maelfu ya waliofurika walitaka angalau hata kuona gari lililobeba mwili wa marehemu ili waamini juu ya kifo chake kwani wengi walikuwa wakiona tukio hilo kama ndoto.
Hali halisi ni kuwa watu walilazimika kujipanga katika Barabara ya Tunisia inayoelekea makaburi ya Kinondoni ili walione japo jeneza tu.

BARUA YA BABA MZAZI
Kabla mwili huo haujapelekwa makaburini, kulitangazwa kuwa kuna barua ya salamu za pole kutoka kwa baba mzazi wa marehemu Kanumba, mzee Charles Kusekwa ambayo ilitakiwa kusomwa mbele za waombolezaji kabla.
Hata hivyo, barua hiyo ilishindikana kusomwa kufuatia watu kuvamia jukwaani na kusababisha isomwe pembeni.
Saa 7:00 mchana mwili wa marehemu Kanumba uliingizwa kwenye gari maalum lililosindikizwa na askari pamoja na farasi wawili ambao walikuwa mbele na nyuma ili kulinda usalama kwa mashabiki waliokuwa na shauku ya kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

MAKABURI YAVUNJWA
Katika hali ya kushangaza umati mkubwa uliokosa nafasi ya kuuona mwili wa marehemu ulihamia katika makaburi ya Kinondoni ambapo watu waliruka ukuta kwani geti la kuingilia lilikuwa limefungwa huku wakikanyaga makaburi ya watu wengine na kuyavunja.
Baadaye geti lilivunjwa na umati ukajazana ndani ya eneo la makaburi, hali iliyowapa wakati mgumu polisi na kulazimika kutumia mbwa, farasi na askari wa FFU ili kufanikisha zoezi la kuuingiza mwili huo kaburini.

MAMIA YA WATU WAZIMIA
Kwa mujibu wa mmoja wa madaktari waliokuwa wakitoa huduma ya kwanza, Nassor Matuzia, watu zaidi ya 200 walizimia kutokana na kukosa hewa, mshtuko na wengine kupandwa na presha ambapo wengi wao wametajwa kuwa ni wanawake ambao walikuwa wakikimbizwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

LULU FEKI NUSURA AUWAWE
Wakati gari lililobeba mwili wa marehemu likiingia eneo la makaburi ya Kinondoni, mbele yake kulikuwa na gari ambalo ndani yake alionekana msichana aliyejifunika kitambaa hali iliyozua zogo kwa waombolezaji wakidhani ni msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Baadhi ya waombolezaji walianza kulikimbiza gari hilo wakitaka kulishambulia ili wamdhuru msichana yule lakini gari hilo liliondolewa kwa kasi huku watu hao wakitulizwa na wenzao kwa kuambiwa kuwa aliyekuwa ndani ya gari lile hakuwa Lulu waliyemlenga bali ni feki.

VIBAKA WAPORA
Kutokana na umati huo, vibaka walitumia fursa hiyo kuwapora baadhi ya watu na kusababisha hali ya amani kuwa ndogo.
Pia, mtu mmoja aligongwa na gari na kufariki katika maeneo ya Barabara ya Kinondoni wakati akikimbilia kwenda kwenye makaburi kwa ajili ya kutaka kumzika Kanumba.
Watu walionufaika na msiba huo ni pamoja na wale waliokuwa wakiuza vinywaji baridi na fulana zilizokuwa na picha ya marehemu.

SHIBUDA KWA NIABA YA BABA KANUMBA
Baada ya mwili wa marehemu kuhifadhiwa kaburini, ulifuatia utaratibu wa kuweka mashada ambapo Mbunge Maswa Magharibi, John Shibuda aliweka kwa niaba ya baba wa Kanumba ambaye alishindwa kufika kutokana na matatizo ya kiafya.

WAGOMA KUONDOKA KABURINI
Pamoja na shughuli nzima kukamilika, baadhi ya waombolezaji waligoma kuondoka kwenye kaburi la marehemu Kanumba hivyo kuzua hofu ya kufukuliwa.

NENO LA Blog
Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki, wasanii, Watanzania na Waafrika kwa kuondokewa na kijana wetu. Kwetu sisi marehemu Kanumba atabaki kuwa shujaa kwa kazi zake za sanaa kwani alikuwa mfano wa kuigwa akiwa mmoja wa vijana watafutaji.

No comments:

Post a Comment

New